24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yamwaga ajira 40,000

*Ni kwa wahitimu wenye shahada za fani mbalimbali

Na RAMADHAN HASSAN

-DODOMA

SERIKALI imetangaza neema ya nafasi za ajira kwa wahitimu 40,000 wa shahada za fani mbalimbali.

Hatua hiyo inatokana na agizo la Rais Dk. John Magufuli, ambaye aliagiza vijana wote wenye elimu ya Shahada ya Kwanza waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) “Operesheni Magufuli”  kupewa ajira katika taasisi mbalimbali za Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk. Laurean Ndumbaro, alisema mwaka huu wa fedha Serikali imetenga zaidi ya nafasi 40,000 za ajira katika kada mbalimbali.

Alisema kuanzia Februari mwakani, wataanza kuajiri rasmi lakini kwa sasa wanaanza kutoa ajira kwa vijana 800  waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

“Katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga nafasi ya ajira zaidi ya 40,000, sasa kabla hatujatekeleza ujazaji wa nafasi hizo tumetoa hii nafasi ya kwanza kwa hawa waliohitimu, kwa hiyo nafasi zipo nyingi za kuweza kuwachukua hawa wote.

“Vijana hao wanaelekezwa kuwasilisha taarifa binafsi (CV) vyeti vya elimu, taaluma na vyeti vya kuhitimu mafunzo ya JKT vilivyothibitishwa na JKT katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili Serikali iweze kuona namna kuwatumia vijana hao katika maeneo mbalimbali Serikalini,” alisema.

Alipoulizwa ni nafasi zipi watazipa kipaumbele katika ajira hizo, Dk. Ndumbaro, alisema ni katika kada za ualimu na afya ambapo kwa upande wa afya alidai kwamba wataangalia uhitaji katika vituo vipya vya afya pamoja na zahanati.

Hata hivyo, alitaja sifa za vijana waliohitimu JKT kuwa ni lazima wawe wametumikia kwa kipindi kisichopungua miaka miwili na kwamba wanatakiwa kuwasilisha taarifa zao binafsi, vyeti vya elimu, taaluma na vyeti vya kuhitimu mafunzo ya JKT katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia barua pepe ya [email protected].

WALIOGHUSHI VYETI

Aidha, Dk. Ndumbaro alitumia fursa hiyo kuwaasa waajiri wanaowarejesha makazini watumishi wa umma walioghushi vyeti vya elimu na taaluma kwa visingizio kwamba waliondolewa kimakosa au waliajiriwa kabla ya Mei 20, 2001 kwa sifa ya Elimu ya Darasa la Saba.

“Serikali haitosita kumchukulia hatua mwajiri yeyote atakayekiuka maelekezo halali yaliyotolewa na Serikali kuhusiana na hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi walioghushi vyeti,” alisema Dk. Ndumbaro

Akizungumzia suala la udanganyifu na upendeleo katika upandishwaji vyeo, Dk. Ndumbaro, alisema kuwa ofisi yake imebaini baadhi ya waajiri kuwasilisha taarifa za uongo Ofisi ya Rais-Utumishi ili kuwapandisha vyeo watumishi kwa lengo la kuwanufaisha baadhi yao bila kuwa na vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia utumishi wa umma.

“Ofisi yangu itaendelea kuwachukulia hatua stahiki waajiri watakaobainika kufanya udanganyifu kwa madhumuni ya kuipotosha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili iweze kutoa vibali vya kuwapandisha vyeo watumishi isivyostahili,”  alisema

16 WAFUKUZWA KAZI

Dk. Ndumbaro, alisema katika kujenga nidhamu kwa watumishi, ofisi yake imewachukuliwa hatua za kinidhamu maofisa 16 kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo kufukuzwa kazi kwa kuomba rushwa kwa watumishi mbalimbali ili waweze kuwasaidia kupandishwa vyeo.

Pia alisema maofisa watatu wamepandishwa vyeo kutokana na utendaji kazi wao wa kuridhisha huku 11 wakipewa vyeti vya pongezi kwa kufanya kazi vizuri.

“Kwa sababu gani watumishi wanatoa fedha, sababu marekebisho ya msharahara hayafanyiki kwa siku moja, sasa wengine wanaitumia fursa hiyo kuwalaghai wafanyakazi jambo ambalo halikubaliki,” alisema.

Licha ya hali hiyo, alisema kuwa taasisi sita zimewasilisha taarifa za uongo za watumishi wao katika zoezi la kuhakiki vyeti vya watumishi hewa ambapo anadai jambo hilo wanaendelea kulifanyia kazi na watawachukulia hatua kali.

MISHAHARA

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo alisema katika mwaka wa fedha 2018/19 watumishi 95,905 wenye sifa wamepandishiwa mishahara yao katika mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara.

“Na taarifa za watumishi 6,000 zilizobakia zinaendelea kufanyiwa kazi na ofisi hii na zitawasilishwa ifikapo Januari 2020,” alisema.

Dk. Ndumbaro, alitoa angalizo kwa watumishi wa umma kwa kuwataka kuwa makini na kundi la matapeli ambao wamekuwa wakipiga simu wakiwataka watoe fedha ili wapandishwe vyeo.

 “Nichukue nafasi hii kuwataarifu watumishi wa umma kuwa wale ambao wamekuwa wakipiga simu na kujitambulisha kwamba wanatoka Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora ni matapeli na wasikubali kutoa fedha watoe taarifa kwetu,” alisema.

Katibu Mkuu huyo aliwataka maofisa utumishi nchini kufanya kazi kwa weledi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma badala ya kuwa chanzo cha kero na matatizo ya kiutumishi.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles