NA JENNIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta, amepata baraka kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye, huku akisubiri ruhusa na baraka za aina hiyo kutoka kwa viongozi na mabosi wa klabu yake ya TP Mazembe ili aweze kujiunga kuichezea klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji.
Samatta aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, mara baada ya kumaliza mazungumzo na Waziri huyo ofisini kwake, baada ya kuomba kukutana naye ili kupewa baraka kutoka kwa Serikali kabla ya kuelekea nchini Nigeria katika kinyang’anyiro cha tuzo za Mwanasoka Bora wa Afrika zinazotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Samatta alisema kuwa mazungumzo yote kati yake na uongozi wa KRC Genk yamekamilika, kinachosubiriwa sasa ni viongozi wa klabu yake ya zamani TP Mazembe kumalizana na wahusika toka Ubelgiji.
“Kila kitu kimemalizika mazungumzo yote yameshafanyika, nasubiri TP Mazembe wamalizane na KRC Genk ili nikaanze kibarua changu nchini Ubelgiji,” alisema Samatta.
Kwa upande wake Waziri Nnauye, alimpongeza mchezaji huyo na kuwataka Watanzania wote kuungana kumuombea ili aweze kutimiza malengo yake kucheza nchini Ubelgiji na kuleta tuzo nyumbani.
“Kwa niaba ya Serikali tunaamini Samatta ataleta tuzo nyumbani, hatua aliyofikia ni kubwa sana ameweza kuitangaza nchi kwa ujumla kushinda kwake ni sifa zaidi kwa nchi yetu.
“Serikali ipo tayari kutoa msaada unaotakiwa kwa wachezaji wote kuhakikisha safari zao na juhudi wanazoonyesha zinafanikiwa,” alisema.
Nnauye alisema nia ya Serikali ya awamu ya tano ni kuifanya michezo kuwa shughuli rasmi ya kiuchumi, ambayo itawaingizia kipato wanaocheza.
“Tatizo kubwa tulilonalo michezo imeingiliwa na wajanja wengi ambao wanatafuna jasho la wachezaji, hili ni tatizo kubwa linalowavunja moyo wachezaji na kuwakatisha tamaa na wakati mwingine kipato wanachopata hakilingani na kazi wanayoifanya,” alisema Nnauye.
Nnauye alieleza kuwa Serikali itahakikisha inatengeneza mazingira mazuri kila mtu apate haki yake na michezo iweze kuliingizia taifa kipato.
Samatta ameingia kwenye kundi la wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa ndani sambamba na nyota wengine 24 wanaocheza soka kwenye klabu mbalimbali barani Afrika.