Serikali yakwama kwa Lissu mahakamani

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, akizungumza na Wakili wake, Peter Kibatala (kushoto) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana. Kulia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema), Said Kubenea.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, akizungumza na Wakili wake, Peter Kibatala (kushoto) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana. Kulia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema), Said Kubenea.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, akizungumza na Wakili wake, Peter Kibatala (kushoto) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana. Kulia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema), Said Kubenea.

* Yamruhusu Wakili Kibatala kumtetea, Jamhuri yatakiwa kukubaliana naye

AZIZA MASOUD NA PAULINA KEBAKI, DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, jana ilitupilia mbali pingamizi lililotolewa na upande wa Jamhuri la kumzuia Wakili Peter Kibatala kumtetea Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi yenye mashtaka matatu.

Lissu ameshtakiwa mahakamani kwa makosa mawili ya uchochezi na moja la kutoheshimu mahakama.

Uamuzi wa kutupilia mbali pingamizi hilo ulitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha ambaye aisema kuwa kwa mazingira yalivyo katika kesi hiyo, mahakama haioni kikwazo cha wakili Kibatala kushindwa kumtetea mteja wake.

Alisema mahakama haoni sheria inayomzuia Kibatala kutoa ushahidi kwa Jamhuri huku akiwa wakili upande wa utetezi.

“Kutokana na mazingira ya kesi hii, mahakama haioni  kikwazo cha wakili wa mtuhumiwa kushindwa kuendelea na kazi yake, nimepitia kanuni za uwakili na  sheria za ushahidi, hakuna kifungu chochote kinachomzuia wakili kumtetea mteja wake kwa kuwa ni shahidi na alikuwepo wakati wa kuchukua maelezo,” alisema Hakimu Mkeha.

Aidha, hakimu huyo alirejea misimamo ya sheria za nchi mbalimbali zinazoendana za zilizopo nchini zikiwemo sheria zinazotumiwa na mataifa ya Uingereza na India na kusisitiza kuwa Jamhuri pia inaweza kumtumia Kibatala kama shahidi endapo itakuwa imekubaliana naye.

Baada ya kutupiliwa kwa pingamizi hilo, Wakili Mkuu wa upande wa Serikali, Faraja Nchimbi, alisema hajaridhishwa na uamuzi huo na kueleza kuwa anasubiri kupata mwenendo mzima wa shauri hilo ili aweze kukata rufaa.

Hoja ya upande wa Jamhuri iliibuliwa Agosti 5, mwaka huu ambapo Lissu alifikishwa mahakamani kwa mara ya tatu kwa makosa ya uchochezi.

Wakili Mkuu wa Serikali, Nchimbi na wenzake watatu akiwemo Wakili Mwandamizi Mutalemwa Kishenyi, Simon Wankyo na Paul Kudushi, walipinga Kibatala kusimama kama wakili katika kesi hiyo baada ya kupitia jalada la kesi na kugundua kuwa Kibatala anafaa kuwa shahidi upande wa Jamhuri na uwepo kama wakili wa upande wa utetezi unaweza kuathiri mwenendo wa kesi.

Wakili Nchimbi alidai kuwa baada ya kupitia maelezo ya wakili huyo, walijiridhisha hakuna namna ambayo wanaweza kukwepa kumuita Kibatala kama shahidi katika kesi hiyo, hivyo kimsimamo na kisheria hata kama yeye hataki atalazimika kutoa ushahidi.

Aliiomba mahakama imwondoe Kibatala kumwakilisha Lissu kwa kuwa wakati kesi inasikilizwa shahidi hatakiwi kuwepo mahakamani hasa wakati mashahidi wengine wakitoa ushahidi.

Akijibu, Kibatala alidai hoja zote dhidi yake hazina mashiko wala sifa za kuitwa pingamizi la kisheria kwa kuwa mawakili hao walitumia maelezo waliyodai kuandikwa na Kibatala polisi hivyo wanapaswa kuithibitishia mahakama kama ni yeye aliyeyaandika.

Aliendelea kujibu kuwa mahakama haiwezi kumwondoa kwa sababu hakuna sheria inayosema iwapo wakili akihojiwa hawezi kumtetea mteja wake.

Kibatala aliiomba mahakama ilinde haki ya mshtakiwa kuwakilishwa mahakamani na kwa kuwa suala hilo linahusu haki ya kikatiba kama inaona ni zito ilipeleke Mahakama Kuu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here