33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YAKUSUDIA KUMALIZA TATIZO LA MAJI MAGU

Na CLARA MATIMO – MAGU             |              


SERIKALI imewahakikishia wananchi wilayani hapa kuwa tatizo la ukosefu wa maji safi na salama litamalizika Februari mwakani.

Kwa muda wa miaka 44, Magu imekuwa ikipata maji safi na salama kwa asilimia 23 kutoka chanzo kilichopo Kijiji cha Busulwa, Kata ya Kahangara, kilichosanifiwa mwaka 1974 wakati ina wakazi 6,000 na sasa wapo 299,757.

Akizungumza mjini hapa jana na wananchi wa Kijiji cha Busulwa, muda mfupi baada ya kukagua mradi wa maji Magu Mjini unaojengwa kijijini hapo, ulioanza kutekelezwa Mei 22, mwaka jana na kutarajiwa kukamilika Mei, mwakani, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa, alisema mradi huo unaogharimu Sh bilioni 12 utakuwa na uwezo wa kusafisha lita milioni 7.25 za maji kwa siku na familia 5,344 zitaunganishiwa huduma hiyo.

“Namwagiza mkandarasi (China Civil Engineering Construction Corporation – CCECC) ahakikishe shughuli za mradi huu zinakamilika hadi kufikia Februari, mwakani ili kuwaondolea adha wakazi hawa,” alisema Mbarawa.

Pia alizindua mradi wa maji Kijiji cha Burugu uliogharimu Sh milioni 192, wenye uwezo wa kuhudumia watu zaidi ya 3,500 lakini waliopo kwa sasa ni 1,800.

“Serikali imedhamiria katika mji huu tatizo la maji kuwa historia,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Magu, Dk. Philemon Sengati, aliwataka wananchi kutunza miundombinu ya maji ili azma ya Serikali ya kumtua mama ndoo kichwani itimie kwa kuwa wakazi wilayani hapa wameteseka kwa miaka mingi.

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (Mwauwasa), Anthony Sanga, alisema watahakikisha miradi yote inayotekelezwa na Serikali inakamilika kwa wakati na kwa ufanisi wa hali ya juu ili iendane na thamani halisi ya fedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles