29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YAKUBALI HOJA YA MKAPA

Na GABRIEL MUSHI – dodoma


SERIKALI imekubali ushauri wa marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wa kufanyika mjadala wa elimu nchini.

Ili kufanikisha hilo, wiki ijayo, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – Tamisemi na yule wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, wanatarajia kuandaa mjadala unaotarajiwa kufanyika mara baada ya kumalizika Bunge la bajeti.

Akijibu hoja zilizotolewa wakati wa kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Naibu Waziri Ofisi ya Rais – Tamisemi, Joseph Kakunda, alisema Serikali haina tatizo katika kuitisha mjadala kuhusu anguko la sekta ya elimu nchini.

“Tamisemi haina tatizo, tumeupokea ushauri huo na wiki ijayo tutakutana ngazi ya manaibu waziri na mwenzangu wa Elimu na baada ya Bunge (Bunge la bajeti kwisha), tunaweza kuitisha huo mjadala kama tulivyoshauriwa na marais wetu wastaafu,” alisema.

 

PROFESA NDALICHAKO

Kwa upande wake, Profesa Joyce Ndalichako, alisema ni kweli kuna changamoto katika sekta ya elimu ambazo Serikali inazifahamu, lakini hilo halizuii baadhi ya wadau kuanzisha mjadala mpana kuhusu anguko la sekta hiyo nchini.

“Suala la mjadala ni la afya kwa sababu linalenga katika kuibua changamoto, kwa sababu kumekuwa na mijadala kama Kigoda cha Mwalimu ambayo imekuwa ikizungumzia kuelekea uchumi wa kati.

“Kuna mijadala mbalimbali imekuwa ikitokea, hivyo niseme kama waziri mwenye dhamana, suala la mjadala linapokewa kwa mikono miwili,” alisema.

Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu bajeti ya Wizara ya Elimu, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alisema kamati imekuwa ikipendekeza mabadiliko kwenye mfumo wa elimu nchini tangu Mei 2016.

Bashe alisema licha ya kamati kupendekeza Serikali kutumia mbinu iliyotumiwa na Rais wa Marekani, Ronald Reagan mwaka 1983, alipofanya uamuzi wa kuunda tume maalumu kuchunguza changamoto ya mfumo wa elimu nchini humo, bado ushauri wao haujafanyiwa kazi.

“Tume hiyo ilikuja na ripoti iliyojulikana kama ‘A nation at Risk, The Imperative for Education Reform’, ambayo ilikuwa ndiyo historia ya mafanikio ya mfumo wa elimu nchini Marekani,” alisema.

Alisema hata Rais mstaafu Mkapa, Novemba 2017, alibainisha wazi Tanzania haijaweka msukumo katika kutafakari upya mfumo wa elimu na kwamba kwa hali ilivyo, tunahitaji kufanya mapinduzi kwenye elimu.

Bashe alisema Machi mwaka huu, Mkapa alibainisha tena kuwa anaamini kuna janga la elimu.

Akinukuu maneno ya Mkapa, Bashe alisema: “Hata ukisoma orodha ya shule zetu za sekondari kwenye ufaulu, katika 10 za kwanza ukiangalia unaweza kuwa na uhakika kuwa nane si za Serikali, ni za watu binafsi na wakati huo Serikali ndio mhimili mkuu wa elimu, lazima tujiulize kuna kasoro gani?”

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles