Na Ramadhani Hassan, Dodoma
SERIKALI imekiri limekuwapo ongezeko la uhalifu unaofanywa na waendesha bodaboda katika maeneo mengi ya Dar es Salaam.
Hayo yalielezwa bungeni jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum Subira Mwaifunga (Chadema).
Mwaifunga alisema limekuwapo wimbi kubwa la uhalifu unaofanywa na baadhi ya madereva bodaboda na bajaji katika maeneo mengi ya Dar es Salaam.
‘’Je Serikali mpaka sasa imechukua hatua gani kudhibiti wimbi hili linalokuwa tishio kwa watumiaji wa vyombo hivyo vya usafiri.
‘’Je Serikali ina utaratibu gani wa kuhakiki na kutambua mmiliki, dereva na mahali zinaegesha bajaji na bodaboda?’’aliuliza Mwaifunga.
Akijibu swali hilo, Mwigulu alikiri na kudai kuwa limekuwapo ongezeko la uhalifu unaofanywa na waendesha bodaboda na bajaji katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mwigulu alisema Serikali kupitia polisi imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kama vile kufanya doria za magari, pikipiki na miguu na kuanzisha na kushirikiana na vikosi vya ulinzi na usalama kubaini na kuzuia uhalifu.
Alisema Serikali kupitia Serikali za Mitaa na Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam zimeendelea kuhakiki pikipiki hizo ikiwa ni pamoja na kuwapangia maeneo ya kupaki.
‘’Kupitia usajili wa TRA na Serikali za Mitaa na Halmashauri za Jiji zimeendelea kuhakiki pikipiki hizo na kuanzisha utaratibu wa kusajili katika maeneo ya maegesho kupata kumbukumbu za miliki, dereva na eneo lake maalum la kuegesha,’’alisema.