29.2 C
Dar es Salaam
Friday, August 19, 2022

Serikali yajivunia sera ya elimu bure

Christina Gauluhanga Na Tunu Nassor -Dar es Salaam

SERIKALI imesema inajivunia sera ya elimu bila malipo ambayo imechangia ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne kutoka asilimia 67 mwaka 2015 na kufikia asilimia 80.67 mwaka jana.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akikabidhi magari 39 kwa vyuo 35 vya ualimu vya Serikali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alisema katika kipindi hicho Serikali imetumia Sh trilioni 1.03 katika kutekeleza mkakati wa elimu bila malipo kwa miaka yote minne.

Alisema mpango huo umesaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa shule ya awali, msingi na sekondari.

“Tunashukuru Serikali tunaweza kutoka kifua mbele kwa sababu mpango wa elimu bure umezaa matunda, hata kama baadhi ya watu wanajifanya hawaoni, lakini ukweli ni kwamba umechangia idadi ya wahitimu na ufaulu nchini,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema kuwa ufaulu wa masomo ya sayansi unaendelea kuongezeka kwa sababu ya kuimarishwa kwa maabara  ambapo zimejengwa zaidi ya 1,500 katika shule mbalimbali nchini zilizogharimu Sh bilioni 16.900.

Akitolea mfano ufaulu kwa masomo ya kemia, Profesa Ndalichako alisema umepanda kutoka asilimia 60 mwaka 2015 na kufikia asilimia 76 mwaka jana.

Akizungumzia kuhusu miundombinu, alisema shule kongwe za Serikali 65 kati ya 88 tayari zimekarabatiwa na kubaki 23 ambazo zinatarajiwa kukarabatiwa mwaka huu.

“Shilingi bilioni 201 zimetengwa za ukarabati shule hizo zilizobaki sambamba na uimarishaji miundombinu na ufundishaji,” alisema Profesa Ndalichako.

Aliongeza kuwa katika mafunzo ya ualimu, Serikali imetumia Sh bilioni 5.5 kununua kompyuta 480, projekta 200 na mashine za kudurufu nyaraka.

“Ili kuendana na kasi ya elimu, tayari wakufunzi 1,273 wamepewa mafunzo ya elimu ya kiteknolojia na habari, ufundishaji masomo ya sayansi na lugha,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema wametumia Sh bilioni 36 kukarabati vyuo vya ualimu ikiwamo Kitandali, Ndala, Shinyanga, Mpuguso na Dakawa pia kukijenga upya chuo cha Kabanga.

Aidha alisema kwa mwaka wa fedha 2019/20 wametenga Sh bilioni 40 kwa lengo la kujenga vyuo vya elimu ya ufundi katika halmashauri 25.

Akizungumzia kuhusu utoaji mikopo ya elimu ya juu, alisema kwa sasa fedha zinatolewa mwezi mmoja kabla ya kufunguliwa kwa vyuo ambapo zilizotengwa ni Sh bilioni 250 na hadi sasa tayari Sh bilioni 240 zimekwishatumika.

“Serikali imetumia hadi sasa zaidi ya  Sh trilioni 1.6 katika kulipia mikopo ya elimu ya juu tangu mwaka 2016 hadi Desemba mwaka jana,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema ili kuhakikisha kunakuwa na udhibiti ubora katika shule na vyuo, tayari wizara yake imejenga ofisi 100 za udhibiti ubora  na magari 45 na nyingine 55 zitajengwa kwa mwaka huu wa fedha.

“Ofisi zote tumenunua vifaa muhimu, ikiwamo mashine ya kudurufu, kompyuta mapakato, printa na magari 45 ambapo mengine 65 yatanunuliwa katika mwaka huu wa fedha,” alisema Profesa Ndalichako.

Aidha ameonya matumizi mabaya ya magari hayo ikiwamo kubeba mizigo isiyostahili, bali yatumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Msiende kuyaua haya magari, mkayape huduma zote kwa wakati, mkishindwa kuyatunza na sisi tutakula sambamba na ninyi,” alionya Profesa Ndalichako.

Akizungumza kwa niaba ya mashirika wadau wa elimu, John Lusingu alisema bado kuna changamoto kadhaa ambazo hazijafanyiwa kazi katika sekta ya elimu.

Alisema ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule mbalimbali ni changamoto kwa sababu ya hitaji la walimu kuongezeka, hivyo wapo tayari kuhakikisha pengo hilo linazibwa.

“Sisi kama wadau wa elimu tutaimarisha ushirikiano na kuhakikisha mpango wa mafunzo kazini wa kuongezea ujuzi walimu unatekelezwa ipasavyo,” alisema Lusingu.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Moshi Kabwenge alisema hadi sasa kuna jumla ya vyuo 35 vya ualimu hapa nchini  vya Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,987FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles