29.7 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YAJALI MASILAHI YA MUDA MREFU SEKTA YA MADINI

Na Mwandishi Wetu-Dodoma


KATIKA kikao kinachoendelea cha Bunge, Serikali imeendelea kusimama kidete kutetea msimamo wake wa kupandisha mrabaha kwani umeonesha kuleta faida na tija kwake kwa kuongezeka kwa kipato.

Hii imedhihirika  kwenye kikao cha Bunge ambapo Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, imeitaka Serikali kupunguza mirabaha inayotoza katika biashara ya madini ili kuepusha utoroshaji rasilimali hizo nje ya nchi  kwenda nchi jirani ambazo zimekuwa zikitoza kiwango kidogo.

Serikali imekomalia mrabaha mkubwa kwani inafaidika na mapato yatokanayo kwa kupanda kinyume na matakwa na hofu ya wabunge ambayo yanatoa suluhisho la muda mfupi na kuwapa ushindi wale ambao wanaoshiriki na utoroshaji huo na hivyo ni kinyume na taratibu.

Ofisa mmoja wa madini anasema kwa sharti asitambulike, kuwa Serikali imeimarisha ulinzi na udhibiti wa ushughulikiaji wa madini na hivyo utoroshaji utapungua kwa kiasi kikubwa na ukamilishaji wa uzio kwenye madini ya tanzanite  kule Mirerani utasaidia  sana kupunguza tatizo hilo.

Anasema nchi za jirani zinazofaidika na madini yetu zinafanya mrabaha mdogo ili kushindana nasi wenye mali na kwa vile mirija hiyo inafungwa, tishio hilo mwishowe litakwisha kwani kimsingi Serikali haifanyi mambo yake kwa vionjo ila kwa misingi na msingi ni kufanya biashara halali na kupata thamani ya kweli ya madini yetu.

Sheria ya Fedha ya Madini iliyopitishwa na Bunge Juni mwaka jana, inawataka wafanyabiashara kulipa asilimia sita ya mirabaha ya madini ikiwa ni ongezeko la asilimia tatu  kwa kiwango kile ilichokuwa wakitozwa awali.

Mwenyekiti wa kikao hicho, Vedasto Mathayo, alisema kuna nchi za jirani ambazo zimekuwa zikitoza mrabaha wa asilimia moja na hivyo watu hupeleka madini huko, kwani wanapata faida kubwa kuliko kuuza nchini madini hayo.

Mathayo alizungumza hayo wakati wa kujadili na kufanya uchambuzi wa  kamati hiyo  kwa bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2018/19.

Mbunge  huyo wa Musoma Mjini (CCM), alidai  kutokana na mrabaha kuwa mkubwa, wachimbaji wadogo wamekuwa wakitumia mwanya huo kutorosha madini kwenda nje ya nchi ambako wanatozwa kidogo.

Naye Naibu waziri wa Madini, Dotto Biteko, alikiri Tanzania kutoza mrabaha zaidi ya nchi jirani, lakini alitetea hali hiyo kutokana na ukweli kuwa athari zinazopatikana  kwa mazingira baada ya wachimbaji kuondoka ni kubwa.

“Lazima kupata mrabaha mkubwa kuziba pengo la hasara hizo zinazopatikana baada ya wawekezaji kuondoka nchini,” alisema Biteko.

Wachunguzi wa mambo wanadai kuwa Kenya imefungua soko la madini nchini mwake na kama halikuzingatiwa vilivyo, litaathiri uhai wa biashara hiyo kwa Tanzania, kwani pamoja na  nchi hiyo kuliita kuwa ni soko la kimataifa, lengo lake ni kutegea madini ya vito yatokayo nchini na yale ya DR Kongo ambayo ni mengi kama Tanzania.

Kwa hali hiyo, Tanzania ipo katika hatari ya kupoteza soko la madini ya vito baada ya Kenya kufuta ushuru wote pindi yanapoingia nchini humo.

Hatua hiyo ya Kenya imefikiwa katika mkutano maalumu kuhusu sekta ya madini (Kenya Mining Forum) uliofanyika jijini Nairobi, Desemba 4 hadi 5, mwaka jana  na kuhudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wake William Ruto na Waziri wa Madini, Dan Kazungu.

Katika mpango mkakati uliotangazwa katika mkutano huo ulioshirikisha wajumbe zaidi ya 200 kutoka mataifa mbalimbali, Serikali ya Kenya ilisema inafungua mipaka yake ili kuruhusu madini ya vito kuingia bila vikwazo vyovyote.

“Kufungua mipaka ya Kenya kuruhusu madini ya vito kutoka Ukanda wa Afrika kuingia Kenya kwa uhuru bila vikwazo,” ilisema sehemu ya mpango mkakati huo.

Pia katika mkutano huo, Serikali ya Kenya ilisema inaunda Shirika la Madini la Taifa huku ikikusudia kulifanya kuwa shirika kubwa la madini barani Afrika.

Mbali na hayo imesema pia itahakikisha linasajiliwa katika masoko makubwa ya hisa duniani, ambayo ni New York Stock Exchange (NSE) na London Stock Exchange (LSE), lengo likiwa ni kupata mitaji ya uwekezaji katika sekta ya madini.

Wakati Kenya ikipanga mikakati yenye lengo la kuifanya  kuwa kitovu cha biashara ya madini ya vito katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Tanzania imekuwa  kinyume  kwa kutoza ushuru kwa madini kama hayo yanayoingizwa nchini  mwake wakati wa maonyesho yanayofanyika jijini Arusha na Mirerani kudai mrabaha mkubwa kwa yale yanayotoka kuuzwa nje.

Madini ya vito yanayoingizwa nchini hutozwa asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na asilimia 25 ushuru kwa bidhaa zinazoingia nchini (import duty) kutokana na ukubwa wa mzigo.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Wanunuzi na Wauzaji Madini Tanzania (Tamida), Sammy Mollel, aliwahi kusema kuwa hatua hiyo ya Kenya ni changamoto kubwa kwa sekta ya madini nchini.

“Hatua ya kuondoa kodi na ushuru (zero rated) kwa madini ya vito yanayoingia nchini humo, kwa kiasi kikubwa kutadhoofisha  maonyesho  na biashara yetu ya madini ya vito ambayo yanasuasua, kwa sababu wafanyabiashara watakwenda Kenya badala ya kuja Tanzania.

Lakini  faida nazo zipo kwani Biteko alisema  bungeni kuwa kutokana na ongezeko la mrabaha huo, makusanyo yameongezeka katika sekta ya madini katika kipindi cha mwaka mmoja.

“Kwa mwaka mmoja tangu imeanza kutumika, sekta ya madini inakua vizuri na imechangia kuongeza mapato,” alisema.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, aliwahi kuripotiwa  akisema kuwa takwimu za makusanyo ya maduhuli zinaonyesha hadi Februari 28, mwaka huu yamefikia asilimia 103.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles