Mwandishi wetu -Pwani
SERIKALI kupitia Wizara ya Nishati, imezindua rasmi mradi mpya wa umeme unaolenga kupeleka nishati hiyo maeneo yaliyoko pembezoni mwa miji.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki mkoani Pwani na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, kwa nyakati tofauti alipokuwa akizindua mradi unaojulikana kwa jina la ‘Peri-Urban’ katika wilaya za mkoa huo na kubainisha kuwa gharama ya wananchi kuunganishwa ni sawa na ile ya umeme vijijini, yaani Sh 27,000.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo wilayani Mkuranga, Dk. Kalemani alisema Serikali iliamua kuandaa mkakati maalumu wa kupeleka umeme maeneo ya pembezoni mwa miji ambayo yalibainika kurukwa na miradi mbalimbali ya umeme.
“Mradi huu ni mahsusi kwa ajili ya maeneo ambayo yako mijini, lakini yana sura ya vijiji; yaani yako pembezoni mwa miji,” alisema.
Alisema Serikali imetumia gharama kubwa kutekeleza mradi huo, hivyo akawataka wananchi katika maeneo yote ambako utatekelezwa, wachangamkie fursa hiyo kwa kujitokeza kwa wingi kulipia ili waunganishiwe umeme kisha wautumie kwa shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo.
“Gharama za kutekeleza mradi huo wilayani Mkuranga ni Sh bilioni 11.5, Wilaya ya Kisarawe Sh bilioni 25 na Wilaya ya Kigamboni Sh bilioni 9.32 ambazo zote ni fedha za ndani.
“Hizo ni wilaya ambako tayari mradi umezinduliwa rasmi, lakini zoezi hilo linaendelea katika maeneo mengine mbalimbali nchini,” alisema.
Katika wilaya hizo tatu ambazo tayari waziri amezindua mradi husika, alitoa maelekezo mahsusi kwa wakandarasi ambao wanatekeleza kazi hiyo.
Miongoni mwa maagizo hayo ni kuhakikisha mradi unatekelezwa ndani ya kipindi kilichoainishwa katika mkataba ambacho ni miezi tisa.
Pia, aliagiza wananchi wenye nyumba zisizozidi vyumba vinne, wagawiwe vifaa vya Umeme Tayari (Umeta), ili kuwapunguzia gharama za kutandaza mfumo wa nyaya za umeme.
Alisema vifaa hivyo vimetolewa bure na Serikali kwa idadi ya 250 kila eneo na kwamba vikiisha, wananchi watauziwa kwa gharama ndogo ya Sh 36,000.