26.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 17, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Serikali yaja na mkakati wa miaka 10 kuimarisha uzalishaji wa ngano

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imeandaa mkakati wa miaka 10 wa kuongeza uzalishaji wa zao la ngano nchini, ikilenga kupunguza utegemezi wa uagizaji wa zao hilo kutoka nje ya nchi.

Akizungumza Februari 18, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha wadau wa zao la ngano, Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Mlola, alisema kuwa sekta ya kilimo inakabiliwa na changamoto ya uzalishaji mdogo wa ngano, ambapo Tanzania huzalisha wastani wa tani 100,000 pekee ikilinganishwa na tani milioni moja zinazohitajika kwa matumizi ya ndani.

Sekta ya ngano ina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi. Tunajua kilimo huchangia asilimia 26 ya Pato la Taifa, huku asilimia 65 ya Watanzania wakiwa wameajiriwa katika mnyororo wa thamani wa sekta hii. Hata hivyo, bado tunaagiza asilimia 90 ya ngano kutoka nje, hali ambayo tunalenga kuibadilisha kupitia mkakati huu wa miaka 10,” amesema Mlola.

Mkakati huo unalenga kuongeza uzalishaji wa ngano kutoka tani 100,000 hadi tani milioni 1.5 ifikapo mwaka 2035. Ili kufanikisha hilo, Mlola alieleza kuwa hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa, zikiwemo usambazaji wa mbegu bora za ngano, ambapo tani 64,266 tayari zimetolewa kwa wakulima.

Aidha, Mlola alisema kuwa upatikanaji wa mbolea umeimarishwa, ambapo hadi Januari 31, 2025, jumla ya tani 247,000 za mbolea zilikuwa zimesambazwa katika mikoa inayozalisha ngano. Serikali pia imewekeza katika miundombinu ya kuhifadhi na kusindika zao hilo kwa kukarabati maghala 15 katika maeneo ya uzalishaji wa ngano na kujenga vituo vitano vya huduma za zana za kilimo.

Pia, juhudi zinaendelea kukamilisha upimaji wa afya ya udongo kwa ajili ya kuandaa ramani ya udongo nchini. Vilevile, serikali imepanga kuendeleza skimu za umwagiliaji katika mashamba yenye ukubwa wa hekta 100,000 ili kuongeza tija kwenye uzalishaji wa zao hilo.

Hata hivyo, Mlola alibainisha kuwa bado kuna changamoto katika kilimo cha mkataba kati ya wakulima, wanunuzi na wasindikaji, kutokana na kukosekana kwa kanuni za kusimamia mikataba hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mazao na Ubora, Kamwesige Mutembei, alisema kuwa kikao hicho cha wadau kililenga kuweka mipango ya muda mfupi na wa muda mrefu ili kuendeleza zao la ngano nchini.

Naye mkulima wa ngano kutoka Kilimanjaro, Isaya Mollel, alieleza kuwa changamoto ya masoko bado ni kubwa, kwani kuna mteja mmoja pekee wa zao hilo katika eneo lao, hali inayosababisha ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima.

Mkakati huu wa serikali unatarajiwa kuleta mapinduzi kwenye sekta ya ngano na kupunguza utegemezi wa uagizaji wa zao hilo kutoka nje, hatua ambayo pia itaongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
595,000SubscribersSubscribe

Latest Articles