24 C
Dar es Salaam
Thursday, July 25, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaitaka TWCC kuwafikia wanawake waliko vijijini

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Serikali imeitaka Taasisi ya Chama cha Wanawake wafanya Biashara Tanzania (TWCC), kuhakikisha inakuwa mstari wa mbele katika kuwafikia wanawake walioko vijijini ambao wamekuwa wakipitwa na fursa mbalimbali kutokana na mazingira yao hali inayo dumaza jitihada za kumkomboa mwanamke.

Mwenyekiti wa TWCC Taifa, Mercy Silla akizungumza alipokuwa akitoa hotuba yake ya utangulizi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mhe. Waziri, Dk. Doroth Gwajima kuzungumza

Agizo hilo limetolewa Dar es Salaam Juni 9, 2022 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Ushiriki wa Makundi Maalum kwenye Manunuzi ya Umma.

Dk. Gwajima amesema serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imekuwa mstari wa mbele kuandaa mazingira wezeshi ya kumkomboa mwanamke lakini fursa nyingi zimekuwa zikibakia kwa wachache waliopo mijini na kundi kubwa ambalo linafikia asilimia kubwa ya uzalishaji mali katika shughuli za kilimo likibaki bila taarifa sahihi.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, akizindua Ripoti ya ushiriki wa Makundi Maalum katika Manunuzi ya Umma uliofanyika kwenye Hoteli Sheraton jijini Dar es Salaam.

“Nitoe wito sasa kwa ndugu zangu wa TWCC, kwakuwa ninyi tayari mnamtandao mpana uliopo nchi nzima, mtumie fursa hiyo kuwafikia wanawake waliowengi ambao wapo maeneo ya vijijini hawa bado fursa nyingi hawazifahamu.

“Hivyo mkitumia vizuri jukwaa lenu la TWCC, naimani wengi watapata mwamko na kushiriki katika mambo mbali mbali mathalani haya ya zabuni,” amesema Dk. Gwajima.
Aidha, Dk. Gwajima ameeleza kuwa serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya kuwezesha wanawake kiuchumi.

“Uwepo wa mifuko rasmi ya uwezeshwaji kiuchumi ikiwemo mfuko wa maendeleo ya wanawake (WDF), TASAF, Mfuko wa Rais wa Uwezeshaji na mifuko mingine ni kielelezo kuwa serikali inawajali wanawake.

“Mwaka 2016 serikali ilifanya mabadiliko ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2011 katika Kifungu cha 64 (a) katika kipengele cha 2 kwa kutoa nafasi kwa makundi maalum kuwezeshwa kushiriki katika fursa za manunuzi ya umma iliyotaka kutengwa asilimia 30 ya bajeti yake kwa ajili ya makundi maalum wakiwepo wanawake,” amesema Dk. Gwajima.

Mkurugenzi wa TWCC Mwajuma Hamza akizungumza alipokuwa akitoa ukaribisho kwa mgeni rasmi na wadau mbalimbali walishiriki Kikao hicho.

Upande wake Mwenyekiti wa (TWCC) Taifa, Mercy Silla ameipongeza serikali na kuomba jitihada hizo ziongezwe kwani wanawake walio wengi wanachukua mikopo wakiwa hawana maarifa ya biashara au shughuli wanayotaka kuifanya hivyo kuishia kufilisika.

“Kwanza kabisa tunampongeza Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha jitiahada za makusukudi na kwa vitendo za kutaka kuona wanawake wa Kitanzania wanajikomboa kiuchumi ikiwa ni pamoja na kutoa fursa mbalimbali zikiwemo mikopo ya Halmashauri.

“Mheshimiwa Waziri pamoja na washiriki bado ipo changamoto kwa wanawake wanaochukua mikopo ikiwepo masharti ya kukopa ambayo husisitiza kuwa kikundi cha watu jambo hili kwa namna moja linakwamisha jitihada za mtu mmoja mmoja, kwakuwa kila mtu anakuwa na mawazo tofauti hivyo hata wakichukua Mikopo wanashindwa kuelewana, lakini kama masharti yatabadilika itawezesha kila mwenye wazo lake ataweza kufanya anachoweza,” amesema Silla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles