29 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 31, 2023

Contact us: [email protected]

Serikali yaibana Benki ya Stanbic

Pg 1*Ni kuhusu ufisadi wa kimafia wa trilioni 1.3/- za mkopo

*Kulipa faini ya mabilioni, vigogo wake wahojiwa

Na Jonas Mushi, Dar es Salaam

HATIMAYE Serikali imetangaza kuchukua hatua dhidi ya Benki ya Stanbic Tanzania, kutokana na kashfa iliyohusisha upatikanaji wa mkopo wa Serikali.

Hatua hiyo imelenga kujua watu waliofaidika na rushwa ya Sh bilioni 12 zilizolipwa kwa Kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors (EGMA), kupitia benki hiyo.

Katika uamuzi huo, Serikali imeitaka benki hiyo kulipa faini ya Sh bilioni tatu, kwa kujihusisha kufanya malipo kwa kampuni hiyo kinyume cha sheria.

Wakati Serikali ikichukua uamuzi huo taarifa za ndani ziliiambia MTANZANIA kuwa, vigogo waliohusika na ufisadi huo wameshahojiwa na vyombo vya dola tangu Desemba mwaka mjana kwa hatua zaidi za kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema baada ya uchunguzi waligundua kulikuwa na mapungufu ya benki hiyo katika kufanya miamala iliyoihusisha EGMA na kwamba haikuweka utaratibu madhubuti wa udhibiti wa ndani.

“Sheria inaitaka Benki ya Stanbic kutoa utetezi katika kipindi cha siku 20 ambacho kitaishia Januari 30, mwaka huu na endapo Benki Kuu haitaridhika na utetezi, benki ya Stanbic italazimika kulipa faini hiyo,” alisema Dk. Mpango ambaye alikuwa ameandamana  na Naibu Gavana, Lila Mkila katika mkutano huo.

Alisema Benki Kuu imechukua hatua hizo kama onyo kwa Benki ya Stanbic ili iweze kuwa makini katika kuhakikisha kuwa shughuli zake zinaendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kibenki na kuzingatia sheria.

Akielezea namna BoT ilivyofanya uchunguzi katika benki hiyo, Dk. Mpango,  alisema Julai mwaka 2013 BoT kupitia ufuatiliaji wa kawaida wa shughuli za mabenki, iligundua matatizo yaliyohusiana na hasara itokanayo na mikopo na pia matatizo ya kuacha na kuondolewa kazini kwa viongozi waandamizi wa Stanbic katika muda mfupi.

Alisema kutokana na hali hiyo BoT iliamua kufanya ukaguzi wa kulenga  katika benki hiyo kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu 47 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 na kifungu cha 31 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

EGMA ni kampuni ya kitanzania iliyohusika katika uwezeshaji wa upatikanaji wa mkopo wa Serikali wa Sh trilioni 1.3 na inatuhumiwa kupokea kiasi cha sh bilioni 12 kama rushwa kwa kuwezesha upatikanaji wa mkopo huo.

MATOKEO YA UKAGUZI

Waziri huyo alisema katika ukaguzi huo, wakaguzi wa Benki Kuu pamoja na mambo mengine walibaini miamala ya kutia shaka iliyohusu malipo kwa Kampuni ya EGMA ambapo Standard Bank Plc (ambayo kwa sasa inajulikana kama ICBC Standard Bank) na Stanbic Bank Tanzania Limited kwa pamoja walikuwa “mwezeshaji mkuu” (Lead Arrager).

Alisema malipo hayo yalifanyika kinyume na taratibu za kibenki kwani fedha hizo zilitolewa kwa muda mfupi na kwa njia ya fedha taslimu.

“Malipo hayo kwa kampuni ya EGMA yalikuwa yamefanyika kinyume cha taratibu za kibenki na yalihusisha uongozi wa benki ya Stanbic na jumla ya malipo yalikuwa ni kiasi cha dola za kimarekani milioni 6 na zililipwa katika akaunti ya EGMA na kutolewa kwa muda mfupi kwa njia ya fedha taslimu ambayo ni nje ya taratibu za kibenki,” alisema Dk. Mpango.

Alisema baada ya uchunguzi taarifa za ukaguzi huo iliwasilishwa kwa benki ya Stanbic kwa mujibu wa taratibu na Benki Kuu iliagiza Bodi ya Wakurugenzi aya benki hiyo kuchukua hatua za kurekebisha kasoro zilizoonekana.

BARUA KUTOA UINGEREZA

Dk. Mpango, alisema Septemba 29, mwaka jana Benki Kuu ya Tanzania, ilipokea barua kutoka Idara ya Serikali ya Uingereza inayohusika na Upelelezi wa Makosa ya Kughushi na Rushwa (Serious Fraud Office-SFO) ikiiomba Benki Kuu ruhusa ya kutumia ripoti yake ya ukaguzi kama ushahidi katika kesi dhidi ya Standard Bank Plc ambayo ilikuwa ni mashirika wa Stanbic Bank Tanzania katika kuwezesha mkopo kwa serikali.

Alisema Benki Kuu iliijibu SFO kuwa kwa mujibu wa Sheria za Benki Kuu zinatolewa tu kwa benki au taasisi ya fedha inayohusika na kueleza kuwa benki kuu haikuwa na pingamizi kwa SFO kutumia taarifa za ripoti hiyo kwa kuzingatia chanzo cha ripoti hiyo.

“Hatimaye, Standard Bank Plc ilikubali makosa na ilitozwa faini ya jumla ya dola za kimarekani milioni 32.20 ambapo kiasi cha dola za kimarekani milioni saba zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania, dola milioni 6 ikiwa ni fidia na dola milioni moja ikiwa ni riba,” alieleza Dk. Mpango.

Akizungumzia kuhusu watuhumiwa wengine waliohusika katika sakata hilo, Dk. Mpango alisema Benki Kuu kwa kupitia kitengo chake cha Financial Intelligence Unit (FIU)kinafanya uchunguzi na pale kinapobaini makosa ya rushwa na ukwepaji wa kodi kinapeleka taarifa kwa taasisi husika ili zifuatilie tuhuma hizo.

“Sisi kama Benki Kuu si wataalamu wa masuala ya rushwa au kodi ila ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango tuna kitengo cha Financial Intelligence Unit ambacho kinafanya uchunguzi na kinapobaini uwepo wa rushwa tunapeleka taarifa Takukuru na kama kuna ukwepaji wa kodi tunapeleka taarifa TRA  ili wafuatilie,” alisema.

Alisema FIU inaendelea na uchunguzi wake ili kubaini makosa mengine yaliyofanyika na hatua zitachukuliwa kwa wote waliohusika.

ONYO KWA MABENKI

Waziri huyo wa Fedha, alitumia fursa hiyo kutoa onyo kwa mabenki na taasisi za fedha akizitaka zisijihusishe na makosa ya aina hiyo ambayo ni kinyume cha utaratibu wa kibenki na uvunjaji wa sheria za nchi.

“Hatua hii ni onyo kwa mabenki na taasisi za fedha zisijishughulishe na makosa ya aina hii…hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa benki au taasisi ya fedha yoyote itakayobainika kwenda kinyume na taratibu na sheria za kibenki,” alisema.

KESI ILIVYOANZA

Mwenendo wa kesi iliyotolewa hukumu Novemba 30 nchini Uingereza, unasema tangu mwaka 2011 Serikali ya Tanzania ilifanya juhudi za kupata mkopo wa miradi ya miundombinu kupitia soko la kimataifa la hati fungani bila mafanikio kutokana na kile kilichoelezwa ni kukosa vigezo.

Mwenendo huo unasema, benki ya Standard na Stanbic kwa pamoja zilichukua jukumu la kutafuta mkopo huo kwa Serikali ya Tanzania kupitia waziri wa fedha wa wakati huo (Mustafa Mkulo).

Katika barua pepe ya Februari 25, 2012, Kaimu Mkuu wa Masuala ya Uwekezaji wa Stanbic, Shose Sinare, aliwafahamisha watu fulani ndani ya Standard na Stanbic, akiwamo Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ya Madeni ya Masoko ya Mitaji wa Standard na Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic, kwamba wazo lao limekubaliwa na waziri wa fedha.

Kwa herufi kubwa na maandishi manene, Sinare ambaye kwenye mwenendo wote huo ametajwa kwa nafasi yake bila kugusia jina lake, alibainisha kwamba watapata asilimia 1.4 kama ada ya kuwezesha mpango huo kwa Serikali ya Tanzania.

Mwenendo huo unasema kuwa Mei 2012, kabla ya wazo la mpango huo kusainiwa, Waziri wa Fedha, Mkulo aliondoshwa na nafasi yake kuchukuliwa na waziri mwingine (Dk. William Mgimwa).

Kuanzia Mei 2012 kuelekea mwishoni mwa mwaka 2012, Standard na Stanbic zilijaribu kufufua mpango huo kupitia juhudi zilizofanywa na Sinare na Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic (Bashir Awale), ambao walikutana na maofisa wa Serikali nchini Tanzania.

Mkuu wa Kimataifa wa Madeni ya Mitaji ya Masoko alikuwa akifahamishwa hatua kwa hatua ya maendeleo hayo na Standard, pamoja na timu ya ndani ya ushauri iliyohusika kuandaa nyaraka za mpango huo.

Juni 2012, Sinare aliwasilisha kwa ofisi ya waziri wa fedha  nakala ya mpango huo, ukiendelea kuonyesha Standard na Stanbic kwa pamoja kama maneneja viongozi wa mpango huo, wakitarajia kupokea ada ya asilimia 1.4 ya sehemu ya mkopo huo.

MTOTO WA WAZIRI ALIVYOAJIRIWA

Julai 2012, Stanbic ilimwajiri mtoto wa kiume wa waziri huyo mpya wa fedha.

Agosti 29, 2012, Sinare alimwandikia barua pepe Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ya Madeni ya Masoko ya Mitaji wa Standard, kwamba yeye na Bashir wamefikia ‘mahali pazuri’ baada ya mkutano mzuri na waziri wa fedha na timu yake, na kwamba kwa sasa wako katika mwelekeo mzuri wa kusaini makubaliano ya mpango huo.

Mwenendo wa kesi hiyo unasema Sinare pia alimfahamisha Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ya Madeni ya Masoko ya Mitaji wa Standard, kwamba mkutano na Waziri wa Fedha ulithibitishwa utafanyika Septemba 18.

EGMA ILIVYOINGIA

“Suala hili jipya kwa mujibu ya barua ya pendekezo la mpango huo lilikuja na ada mpya ya asilimia 2.4 ya mkopo wa dola milioni 600 Tanzania ilizoomba. Nyaraka hizo pamoja na mambo mengine zilieleza Meneja Kiongozi ni Stanbic na Standard, kwa kushirikiana na mshirika wa ndani.

“Kwamba Stanbic imlipe mshirika wa ndani, ambaye Standard ilibaini baadaye kuwa alikuwa EGMA, ada ya asilimia moja ya mkopo, kutoka jumla ya ada ambayo iliongezwa kutoka asilimia 1.4 hadi asilimia 2.4,” unaeleza mwenendo wa kesi hiyo.

Mwenendo huo unasema katika barua ya Septemba 20, 2012, kutoka kwa Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ya Madeni ya Masoko ya Mitaji wa Standard kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic na Kaimu Mkuu wa Uwekezaji wa Stanbic, alieleza kwamba wanafanyia kazi barua ya upande wa pili baina yao na washirika wao, kuonyesha namna ada itakavyogawanywa na wajibu wa kila mmoja katika suala hili.

Mwenendo huo unasema kuwa wakati timu ya mkakati ya Standard ilipomjibu Sinare kwamba mshirika wa ndani (Kampuni ya EGMA) anahitaji kusaini barua ya dhamana, Sinare alijibu huku nakala ikienda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Stanbic na Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ya Madeni ya Masoko ya Mitaji, kwamba: “Hapana. Lengo ni kuwaleta kupitia makubaliano ya pembezoni baina yetu na mshirika.

SEKESEKE LA MGAWO

“Kwamba Stanbic itailipa EGMA mgawo wake wa asilimia moja na kugawa mgawo mwingine uliobakia wa ada ya 1.4 kwa Standard.

“Kutokana na makubaliano hayo, Standard haikuwa mtia saini wa makubaliano ya ada hiyo na EGMA. Katika mawasililiano mengine ya simu Septemba 26, 2012, washiriki hao hao watatu walikubaliana kwamba kwa vile EGMA haitahusika kwa vyovyote kama Meneja Kiongozi, inahitaji kutotajwa kabisa katika barua ya dhamana ya kuendesha mpango huo na Serikali,” unaeleza mwenendo huo.

WAMILIKI WA EGMA

Desemba Mosi mwaka jana, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Sefue,  aliwataja wamiliki wa EGMA kuwa ni aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Harry Kitilya, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Mitaji Tanzania, Fratern Mboya na Mkurugenzi Gasper Njuu.

Kutokana na hali alitoa mwito kwa wamiliki hao, kutoa ushirikiano wakati wa uchunguzi wa sakata hilo na kwamba mara baada ya uchunguzi kukamilika, iwapo kutabainika makosa ya rushwa au mengine, sheria itachukua mkondo wake.

“Ombi letu na ombi la Rais John Magufuli watu hawa wanatakiwa kutoa ushirikiano na pengine ameongezeka mmiliki kwenye kampuni hiyo, wahakikishe wanatoa ushirikiano,” alisisitiza Balozi Sefue.

Akizungumzia sakata hilo, Balozi Sefue alisema sio jambo geni kama ambavyo baadhi ya vyombo vya habari nchini vimeripoti kwamba tangu mwaka 2013, Tanzania inalifahamu na ndiyo iliyolipeleka SFO kuchunguzwa.

Akifafanua, alisema katika mwaka 2012/13, Serikali ilifanya utaratibu wa kawaida unaofanywa na nchi mbalimbali duniani wa kukopa kwenye taasisi za benki ambapo Benki ya Standard ilikubali kuikopesha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,212FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles