25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YAHARIBU MIUNDOMBINU SHAMBA LA MBOWE HAI

 

 

Na OMARI MLEKWA-HAI

SERIKALI wilayani Hai  Mkoa wa Kilimanjaro, imeondoa miundombinu ya uzalishaji katika shamba la Kilimanjaro Veggies linalomikiwa na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe  (Chadema).

Miundombinu hiyo iliondolewa jana kwa vile shamba hilo liko ndani ya chanzo cha maji ya Mto Weruweru.

Pamoja na kuondoa miundombinu hiyo, Serikali imemtaka Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema   alipe Sh milioni 18 kutokana na uharibifu wa mazingira aliofanya kwenye chanzo hizo.

Pia, Mbowe ametakiwa kulipa gharama zote zilizotumika kuondoa miundombinu kwenye shamba hilo.

Uamuzi huo umefikiwa  baada ya Mbowe kudaiwa kukaidi amri aliyopewa na Serikali ya kusimamisha kilimo cha mboga mboga katika eneo hilo lenye ukubwa wa ekari mbili, lililopo Kijiji cha Nshara.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gellasius Byakanwa, alisema wameamua kuondoa

miundombinu yote iliyokuwa ikitumika kwenye shamba hilo baada ya Mbowe kupewa miezi minne kuiondoa kwa hiari na kushindwa kutekeleza agizo hilo.

“Januari 23 mwaka huu, Freeman Mbowe, alifika ofisini kwangu akiwa na wanasheria wake kutokana agizo nililotoa kwa ajili ya kusimamisha shughuli za  binadamu katika shamba lake hilo.

“Tulikubaliana atatumia miezi minne kuondoa mazao yaliyokuwa kwenye shamba hilo na miezi minne hiyo imeishia Mei 23, mwaka huu.

“Huyo ni kiongozi na ni kioo cha jamii, haipendezi kufanya vitu kama hivi kwa sababu pia wajibu wa wananchi ni kutunza vyanzo vya maji,” alisema Byakanwa.

Mkaguzi wa Mazingira wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC), Kanda ya Kaskazini, Novatus Mushi, alisema uamuzi waliochukua unatokana na Mbowe kushindwa kufuata sheria ya mazingira ya mwaka 2,004.

Alisema kifungu 81 kinamtaka kila mtu anayeanza mradi wa kilimo kufanya tathinimi ya uharibifu wa mazingira lakini mmiliki huyo hakufanya na wala hakushirikisha mamlaka husika.

“Mmiliki huyo alikiuka sheria ya mazingira kifungu cha 51 kinachokata mtu yeyote yule kutokufanya shughuli za mazingira ndani ya eneo  la mita 60 kando ya chanzo cha maji lakini mtu huyo amefanya hivyo alivyotakiwa kuondoa amekaidi.

“Pia kifungu namba 200 b cha sheria ya mazingira kinataka mtu yeyote yule anayepewa mazingizo na mamlaka  za nchi ikiwamo kukataza shughuli za  binadamu ndani ya maeneo yanayolindwa kisheria afanye hivyo kwa mujibu wa muda aliyopewa na mamlaka husika.

“Huyo bwana alipewa miezi minne aondoke kwa hiari yake na ofisi ya mkuu wa wilaya hakufanya hivyo mpaka leo hii tunapochukua hatua  bado shughuli za uzalishaji zilikuwa zikiendelea katika shamba hili.

“Kwakifupi ni kudharau mamlaka sababu ni mamlaka iliyopo kisheria na imempa agizo lilipo kisheria

“Pia sisi tulimwandikia barua Juni 6 mwaka huu ikimkumbusha asimamishe shughuli za binadamu katika eneo hilo, ambayo iliambatana naadhabu ya kumtaka kulipa Sh milioni 18 kutokana uharibifu wa mazingira katika chanzo hicho maji cha mto Weruweru,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles