27.1 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

SERIKALI YAFUTA ADA ELEKEZI

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.

NA HADIA KHAMIS, DAR ES SALAAM

SERIKALI imesisitiza kufutwa kwa mchakato wa kutangaza ada elekezi kwa shule zote binafsi na udhibiti wa ada hizo sasa utafanywa na Kamishna wa Elimu na Idara ya Ukaguzi.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo aliiambia MTANZANIA ofisini kwake jana kuwa baada ya kupokea maoni ya wazazi, walikaa kikao na Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii Mei mwaka jana ambapo waliamua suala la ada elekezi libaki mikononi mwa mzazi na mmiliki wa shule.

““Suala la ada elekezi lilikwishafutwa na Serikali katika tamko lilitolewa na Waziri wa Elimu yeye mwenyewe katika kikao cha Bunge kilichofanyika Mei 27 mwaka jana na kuamuru suala la ada elekezi  lisijadiliwe tena,”alisema Dk Akwilapo.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema mzazi yeyote atakayetaka kumpeleka mtoto wake katika shule zisizokuwa za Serikali ni uamuzi wake kwa sababu atakuwa ameshakubaliana na ada iliyopangwa.

Alisema kwa sasa wizara hiyo imeboresha shule zote za Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa elimu bure kwa wanafunzi wote.

TAMONGSCO wanena

Akizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wamiliki  na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyo vya Serikali Tanzania (TAMONGSCO) Benjamin Mkonya alipongeza hatua hiyo, huku akisisitiza kuwa suala la ada elekezi ni sawa na suala la kifamilia.

“Suala la upandaji wa ada ni makubaliano baina ya mzazi na mmiliki. Waziri alisisitiza kuwa suala la ada kwa shule zisizokuwa za Serikali hataliingilia,”alisema Mkonya.

Alisema upandishwaji ada kwa shule zisizokuwa za Serikali inategemea na aina ya mahitaji anayoyapata mtoto shuleni na wakati mwingine wazazi wenyewe ndio hutoa oda ya namna mtoto anavyotaka aishi akiwa shuleni.

“Kama mtoto anapewa chakula kizuri, mahitaji mazuri shuleni ni sababu gani itakayosababishwa ashindwe kufaulu, kwa mzazi anayetaka mtoto wake apate elimu bora ni lazima atampeleka katika shule anayoona inafaa,”alisema Mkonya.

Akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara hiyo bungeni Mei mwaka jana, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema mchakato huo umefungwa baada ya kujadiliana na wamiliki wa shule na Kamati ya Bunge.

Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, usimamizi wa utoaji wa michango na ada holela katika shule hizo utashughulikiwa kwa mujibu wa sera, ambapo kutatakiwa kuwepo kwa kibali kwanza.

Alisema kutokana na hatua hiyo ya Serikali, ambayo inalenga kupata muda wa kutafakari suala hilo na kutafuta namna bora ya udhibiti, sasa hakutakuwa na ada elekezi ila michango itadhibitiwa.

Kabla ya tamko hilo, baadhi ya wabunge walipinga mchakato huo na kutaka Serikali kujikita katika kuboresha shule zake na kuachana na utoaji wa ada elekezi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles