30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yafunguka kodi Sh trilioni 424 ya ‘makinikia’

PATRICIA KIMELEMETA

SIKU Chache baada ya Kampuni ya Acacia kuonyesha kushitushwa na deni lililoelekezwa kwenye kampuni tanzu zinazodaiwa kodi ya dola za Marekani 190 (Sh trilioni 424) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), serikali imesema kama hairidhiki iende kwenye bodi ya rufaa ya kodi.

Kampuni hizo ni  Bulyanhulu Gold mine (BGML) inayoendesha mgodi wa Bulyanhulu na Pangea Minerals (PML) inayosimamia mgodi wa Buzwagi,.

Serikali pia imeelezwa kushangazwa na jinsi Acacia ilivyojiingiza kwenye suala hilo ikizingatiwa TRA ilipeleka madai ya kodi hizo kwa  BGML na PML.

Wakati hayo yakiendelea, Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC),   limeripoti kuwa  baada ya Acacia   kutoa taarifa juu ya madai ya kodi iliyoainishwa   na TRA, jana asubuhi kwenye soko la hisa la London, hisa za kampuni hiyo ziliporomoka kwa asilimia 7.7.

Taarifa ya TRA kuzidai kampuni hizo matrilioni ya shilingi  imetolewa  ikiwa ni miezi michache baada ya Kamati ya Rais iliyoongozwa na Profesa  Nehemiah Osoro, kutoa taarifa yake   kuonyesha Acacia imekuwa ikiibia serikali  fedha nyingi kwenye mchanga wa dhahabu (makinikia) unaosafirishwa nje ya nchi.

Ilionyesha pia kuwa Acacia inaendesha shughuli zake nchini kinyume cha taratibu kwa sababu haijasajiliwa.

Baada ya taarifa hiyo kutolewa, Juni 14, Rais Magufuli alikutana na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation Profesa John Thornton,    Dar es Salaam.

Baadaye Ikulu  ilitoa taarifa kuwa Barrick inayomiliki zaidi ya asilimia 60 ya migodi hiyo, ilisema  ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Wizara ya Fedha na Mipango, Beny Mwaipaja, alisema deni hilo ni halali na lilikokotolewa kwa mujibu wa sheria  na endapo wadaiwa wana tatizo, wanajua sehemu ya kwenda.

“TRA iliwasilisha deni hilo kwa kampuni za Bulyanhulu na Pangea na wala siyo Acacia, kama wanaona wameonewa, wawasilishe malalamiko yao kwa Kamishna wa TRA au bodi ya rufani za kodi, yatafanyiwa kazi,”alisema Mwaipaja.

Alisema kampuni za uwekezaji zinajua utaratibu wa kufuata kama zinaona kuna tatizo, hivyo basi Acacia ina muda wa kutosha wa kuwasilisha malalamiko yake kwenye mamlaka zinazohusika kuliko kulalamika bila ya kufuata utaratibu.

“Kila mgodi umepelekewa bili yake kasoro Acacia ambao bado hawajapelekewa bili,”alisema.

Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amesema   masuala yanayohusu mlipakodi, kwa mujibu wa sheria Mamlaka  hairuhusiwi kuyajadili hadharani bali huwasiliana na mhusika moja kwa moja.

“Issue (suala) za mlipakodi kisheria haturuhusiwi kuzi-discuss in public (kuzijadili hadharani) huwa tunawasiliana na mlipakodi moja kwa moja,”alisema Kayombo.

Taarifa ya ACACIA

Taarifa ya Acacia juzi ilisema TRA  inaonyesha kuwa migodi yake ya Bulyanhulu inadaiwa kodi ya kati ya mwaka 2000 hadi 2017  wakati Pangea inadaiwa kodi ya kati ya 2007-2017.

Taarifa yake inasema uchambuzi uliofanywa na TRA umeonyesha Mgodi wa Bulyanhulu unadaiwa dola za Marekani bilioni 154 (Sh trilioni 344.8) na Mgodi wa Pangea dola bilioni 36 (Sh trilioni 76.1).

Inasema dola bilioni 40 (Sh trilioni 89.5 trilioni) ni malimbikizo ya kodi na dola bilioni 15 (Sh trilioni 335.9) ni adhabu na riba.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyochapishwa kwenye tovuti ya kampuni hiyo, kodi hiyo imetokana na ripoti za kamati mbili za Rais zilizoonyesha kuwa kampuni hizo zimekuwa hazitangazi kiasi halisi cha mapato yake yanayotokana na makinikia.

Hata hivyo, Acacia ilisema inaendelea na msimamo wake wa kupinga matokeo ya kamati hizo ikisisitiza imekuwa ikitangaza mapato yake yote.

Kampuni hiyo ilisema bado haijapata nakala za ripoti za kamati ya kwanza na ya pili zilizowasilishwa kwa Rais Magufuli Mei 24 na Juni 12 mwaka huu.

Ripoti ya Profesa Osoro

Akisoma ripoti ya kamati yake, Profesa Osoro  alisema kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mwaka 1998 hadi Machi 2017, makadirio ya chini yanaonyesha makontena yaliyosafirishwa  nje ya nchi ni 44,277 huku kwa makadirio ya juu ni 61,320.

“Jumla ya thamani ya madini katika makontena 44,077 yaliyosafirishwa nje ya nchi katika kipindi cha mwaka 1998 hadi 2017 kwa kutumia kiwango cha wastani, ni Sh trilioni 132.56 trilioni sawa na dola za bilioni 60.25 au Sh trilioni 229.9 sawa na dola za Marekani bilioni 104.5 kwa kiwango cha juu.

“Thamani ya madini yote katika makontena 61,320

yaliyosafirishwa nje ya nchi katika kipindi kati ya 1998 na 2017, kwa kutumia kiwango cha wastani ni Sh trilioni 183.597 sawa na dola za Marekani bilioni 83.45, kwa kiwango cha juu ni sawa na  Sh trilioni 380.499 ambazo ni dola za Marekani bilioni 144.77,” alisema Profesa Osoro.

JPM kufunga migodi

Julai 21 akiwa mkoani Kigoma, Rais John Magufuli alisema: “Nitasimamia haki siku zote katika maisha yangu na niliwaambia nimeanzisha vita hii ya  uchumi, vita ya  uchumi ni mbaya sana.

“Wakubwa wale huwa hawafurahi, kuna viongozi wengi tu mliona yaliyowapata ni kwa sababu nchi zao zilikuwa na mali.

“Lakini wale wakubwa wakataka kuchezea hizo mali kwa manufaa yao na siyo kwa manufaa ya wananchi wa pale. Walitumia mbinu nyingi za kila aina lakini Mungu wangu ni mwema na Watanzania ni wema watasimama kwa ajili ya taifa hili.

“Ninayoongea nayajua ni matrilioni ya fedha ambayo yameibiwa na kwa sasa   tumewaita waje wafanye mazungumzo (Kampuni Barrick), wamekubali lakini wakichelewachelewa  nitafunga migodi yote.

“Ni mara 10 migodi hii tukaigawana Watanzania wachimbe wawe wanauza tuwe tunapata kodi kuliko kuchimbwa na watu wanaojiita wawekezaji halafu hawalipo kodi.

“Walikuwa wanazungumza mle wanachimba dhahabu, madini machache tu… matatu. Tumegundua mle kuna madini mengii,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:

“Tanzania hii ni nchi tajiri, lakini imekuwa ikiibiwa mno. “Tumechezewa sana, mimi nipo serikalini na mimi ndiye najua siri za serikalini.

“Tumechezewa sana kwa kuibiwa sana mali zetu, kwenye dhahabu huku tumeibiwa mno, ukiyajua yale yaliyokuwa yanafanyike mle unaweza ukalia.

“Anasema hapa tunasafirisha mchanga na Watanzania wote tunaamini tunasafirisha mchanga, mbona hawajaja Kibondo kuchukua mchanga wa hapa, mbona na penyewe tunao?

“Lakini tunaamini wanaupeleka kwenye makontena wanapeleka Ulaya na wakishaenda kuusafisha kule ule mchanga unaobaki wala hawaurudishi… ulikuwa ni utapeli wa ajabu na ni aibu kubwa kuona utapeli huu unafanywa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles