30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yafunga kliniki ya Dk. Mwaka

Dk. Juma Mwaka
Dk. Juma Mwaka

Na HERIETH FAUSTINE, DAR ES SALAAM

SERIKALI imefuta usajili kwa vituo vitatu vya tiba mbadala, kikiwamo Foreplan Clinic kinachomilikiwa na tabibu maarufu nchini, Dk. Juma Mwaka.

Kituo hicho kilichopo Ilala Bungoni, Dar es Salaam, kilikumbwa na rungu hilo kutokana na kukiuka masharti waliyopewa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.

Mbali na kituo hicho, pia vipo vituo vya Fadhaget Sanitarium Clinic kinachoendeshwa na tabibu Fadhili Kabujanja na Mandai Herbal Clinic kinachomilikiwa na tabibu Abdallah Mandai.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Dk. Edmund Kayombo, alisema Dk. Mwaka amefutiwa usajili huo kutokana na kukiuka masharti ya kibali alichopewa kwa kujitangaza kuwa anatoa tiba za kisasa badala ya matibabu ya asili.

“Kutokana na kukiuka masharti waliyopewa na Baraza la Tiba Asilia na Mbadala, tumeamua kuvifutia usajili, hivyo hawatatakiwa kutoa huduma yoyote ya kitabibu,” alisema Dk. Kayombo.

Mbali na hao, matabibu wengine wamepewa barua za onyo, wakiwamo Esbon Baroshigwa wa Kituo cha Aman Herbal  Clinic na Castory  Ndulu kutoka Ndulu Herbal Clinic.

Baraza hilo pia limesimamisha huduma za tiba asili kwa miezi sita katika Kituo cha Sigwa Herbal Clinic kilicho chini ya tabibu Simoni Rusigwa pamoja na Lupimo Sanitarium Clinic kinachoongozwa na John Lupimo.

Dk. Kayombo alisema kuwa matabibu hao waliofutiwa usajili na wengine waliosimamishwa kwa muda, licha ya kuitwa na baraza hilo na kupewa onyo, lakini bado waliendelea kutoa huduma ya matangazo kwenye vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Mwenyekiti huyo, alisema kuwa huduma za tiba asili na tiba mbadala zinagusa zaidi maisha na afya za wananchi moja kwa moja, hivyo si vyema zikaachwa ziendeshwe kiholela bila utaratibu wa kitaalamu na kimaadili.

Tukio hilo la misukosuko kwa Dk. Mwaka ni la pili kutokea. Mwishoni mwa mwaka jana, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk. Hamis Kigwangalla, alivamia kituo cha tabibu huyo na kufanya ukaguzi, huku mwenyewe akidaiwa kuwa alitoroka kupitia mlango wa nyuma.

Hatua hiyo ilitokana na kile linachodaiwa ni utata kuhusu uhalali wa tiba anazozitoa, kutokana na uchunguzi wa vyeti vyake kushindwa kutolewa kwa umma kama ilivyoahidiwa.

Akizungumza na wanahabari Sesemba 14, mwaka jana, Dk. Kigwangalla alisema pamoja na hali hiyo, Serikali ni lazima ifanye uchunguzi dhidi ya tabibu huyo.

ILIVYOKUWA

Desemba 14, 2015, Dk. Kigwangalla alifanya ziara ya kushtukiza kwenye kituo cha Dk. Mwaka ambaye amekuwa maarufu kutokana na matangazo mbalimbali anayotoa kila mara kuhusu tiba anazotoa.

Hata hivyo, baada ya Dk. Kigwangalla kufika kwenye kituo hicho, hakumkuta Dk. Mwaka na wenzake na ndipo alipotoa amri ya kufungwa kwa muda kituo hicho, huku akimtuhumu tabibu huyo na wenzake kumkimbia na kisha akaamuru apeleke vyeti vyake ili vichunguzwe na kuona kama huduma wanazotoa zinakidhi vigezo na ni salama kwa wagonjwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles