MAULI MUYENJWA NA TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM
SERIKALI imekifunga Kiwanda cha Nguo cha Urafiki kutokana na mgomo wa wafanyakazi uliotokea jana wakiutaka uongozi kuwalipa malimbikizo ya madai yao ikiwamo mishahara.
Mkuu wa Wilaya wa Kinondoni, Paul Makonda, alitangaza kukifunga kiwanda hicho hadi Desemba 7 mwaka huu yatakapotolewa majibu ya kuridhisha kuhusu changamoto zilizosababisha mgomo huo.
Mgomo katika kiwanda hicho ulianza wiki kadhaa zilizopita ambako mkuu huyo wa wilaya aliuagiza uongozi kulipa madeni na malimbikizo yote ya wafanyakazi hadi Desemba 1 mwaka huu.
Hata hivyo, hadi jana wafanyakazi walikuwa hawajalipwa wala kupewa taarifa yoyote hali iliyosababisha wagome tena.
“Naagiza kusimamisha shughuli za uzalishaji, kiwanda hakiwezi kuendelea kuzalisha katika mazingira yasiyo salama.
“Naomba tukutane Jumatatu wiki ijayo, nitakuja na majibu ya hatma ya kiwanda hiki.
“Ikiwezekana nitakuja na mtu wa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kuwa kiwanda hicho kipo chini ya wizara hiyo.
“Lakini kikubwa ni kujua matatizo yaliyopo hapa likiwamo suala la malipo yenu. Mtajua mnalipwa lini ingawa naambiwa pia kuwa kuna mashine zilikuja ziongeze uzalishaji lakini tatizo liko palepale… tujue nani anahusika na tatizo hilo,”alisema Makonda.
Alisema atakaporudi kiwandani hapo siku hiyo itajulikana nini kifanyike kuhusu uongozi wa kiwanda hicho unaolalamikiwa kuwa ni tatizo akiwamo Ofisa Utawala, Moses Swai.
Katibu wa chama cha Wafanyakazi(TUICO), Tawi la Urafiki, Florian Makero alisema tatizo lililosababisha mgomo huo ni menejimenti ya kiwanda hicho kupuuza maagizo ya DC Makonda alipokwenda kutatua mgogoro huo mara ya kwanza.
“Menejimenti ilikuwa ikiwabagua watu ambao walitakiwa kulipwa madai yao kinyume na makubaliano kuwa watu wote wanatakiwa kulipwa madai hayo kwa usawa,” alisema.
Wachina wafungiwa ndani
Dalili za kuwapo purukushani jana zilianza mapema asubuhi baada ya juzi wafanyakazi wote kukubaliana kuwahi kiwandani hapo kujua hatima yao.
Baadaye wafanyakazi hao walihamasishana ma kufunga lango kuu la kuingilia kiwandani kwa kutumia mnyororo huku raia wa China ambao ni sehemu ya umiliki wa kiwanda hicho wakizuiwa kutoka ofisini mwao.
Raia mmoja wa China alitaka kutoka kwa nguvu katika ofisi hizo lakini alizuiwa na wafanyakazi.
Polisi wakiongozwa na Mkuu wa Kituo cha Urafiki walijaribu kuwatuliza wafanyakazi hao bila mafanikio ndipo walipoamua kutumia mabomu ya machozi.
Hatua hiyo ilisababisha wafanyakazi wawarushie mawe polisi lakini hali ilitulia baada ya DC Makonda kuwasili kiwandani hapo.