Na Mwandishi Wetu, Â Mtanzania Digital
Operesheni maalumu ya kudhibiti fisi wakali na waharibifu wanaosababisha taharuki mkoani Simiyu imeonesha mafanikio makubwa baada ya fisi 16 kuuawa, hatua inayolenga kurejesha usalama wa wananchi.

Hatua hiyo imetangazwa, Februari 19, 2025, na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Kihongosi amesema serikali ilianzisha operesheni maalumu kwa kushirikiana na Jeshi la Uhifadhi kupitia TAWA, TANAPA, TFS, pamoja na Jeshi la Polisi na wananchi ili kukabiliana na wanyama hao waliokuwa wakileta madhara.
“Tarehe 20 Desemba 2024, baada ya fisi kuvamia wananchi, serikali ilichukua hatua ya kushirikisha vyombo vya ulinzi na kuanzisha operesheni rasmi Januari 25, 2025, kwa lengo la kukomesha tatizo hilo,” amesema Mhe. Kihongosi.
Ameeleza kuwa fisi 16 tayari wameuawa tangu operesheni ianze, hatua iliyosaidia kurejesha utulivu mkoani humo.
“Kwa sasa hali ni shwari, hakuna tena taharuki kama ilivyokuwa awali. Tunawataka wananchi waendelee na shughuli zao za kila siku kwa amani,” aliongeza.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa mkoa amekemea vikali imani za kishirikina zinazoambatanishwa na fisi na kuwataka wanaofuga wanyama hao kuacha mara moja, akibainisha kuwa kumiliki nyara za serikali bila kibali ni kosa kisheria.
Kwa upande wake, Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja, amewataka wananchi, hususan wa wilaya ya Itilima, kuwa waangalifu kwa kuepuka kutembea nyakati za usiku na alfajiri, kwani fisi huonekana zaidi katika muda huo.

“Tunaomba wananchi waendelee kushirikiana na maofisa wa Jeshi la Uhifadhi walioko uwandani, ili kuhakikisha operesheni inaendelea kwa mafanikio zaidi,” amesema Maganja.
Amehakikishia wananchi kuwa serikali imedhamiria kuhakikisha usalama wao na askari wa uhifadhi wanafanya kazi usiku na mchana kudhibiti tishio la fisi.
Wananchi wa Simiyu, hususan wa wilaya ya Itilima, wameshukuru serikali kwa hatua zilizochukuliwa, wakisema kuwa operesheni hiyo imewarejeshea utulivu na amani.
“Tulikuwa tunasumbuliwa sana na hawa fisi, lakini baada ya serikali kuingilia kati na kuweka ulinzi, hali imetulia. Hatujasikia tena fisi wakisababisha madhara, tunashukuru sana,” amesema Mozo Mabula, mkazi wa kijiji cha Mwamunhu, wilayani Itilima.
Serikali imeahidi kuendelea na jitihada za kuhakikisha usalama wa wananchi na kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo mbalimbali nchini.