29.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Serikali yaendelea kutoa ufafanuzi usajili wa simu

Na MAREGESI PAUL

-DODOMA

SERIKALI imesema mwisho wa kusajili laini za simu kwa kutumia alama za vidole ni Desemba 31, mwaka huu, huku wasio na vitambulisho vya taifa wakiondolewa wasiwasi.

Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, alipokuwa akitoa ufafanuzi wa mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Viti Maalum, Felister Bura (CCM).

Katika mwongozo wake, Bura alitaka kujua Serikali itachukua hatua gani kwa wananchi watakaoshindwa kusajili laini zao katika kipindi kilichowekwa  watakapokuwa hawana vitambulisho vya taifa.

”Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetangaza kwamba kuanzia Mei mosi mwaka huu, usajili mpya wa laini za simu utaanza na moja ya masharti yaliyowekwa ili upate usajili, ni kuwa na kitambulisho cha taifa.

”Kwa kuwa wanaohusika na vitambulisho vya taifa ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ambao wako chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujua ni hatua gani zitachukuliwa na Serikali   baadhi ya wananchi watakaposhindwa kupata vitambulisho hivyo.

”Mheshimiwa mwenyekiti, nauliza hivyo kwa sababu baadhi ya wananchi wameshajiandikisha muda mrefu, lakini hadi sasa hawajapata vitambulisho hivyo na kwa hali ilivyo, wanaweza wasivipate haraka na hivyo kushindwa kusajili laini zao za simu.

”Kwa hiyo  mheshimiwa mwenyekiti, naomba mwongozo wako juu ya jambo hili kwa masilahi ya Watanzania wengi,” alisema Bura.

Akijibu mwongozo huo, Nditiye alisema utaratibu wa usajili mpya wa laini za simu uliandaliwa tangu mwaka jana kwa kuzingatia mambo mbalimbali.

”Ni kweli alichosema mheshimiwa Bura  kwamba makampuni yote ya simu yameagizwa kusajili laini za simu kwa kutumia alama za vidole.

”Chini ya utaratibu huo, usajili utaanza rasmi Mei mosi mwaka huu na itakapofika Septemba 30, mwaka huu, tutafanya mapitio   kuona jinsi hatua  inavyokwenda.

”Kwa hiyo, itakapofika Desemba 31, mwaka huu, laini zote ambazo zitakuwa hazijasajiliwa kwa kutumia alama za vidole, zitazimwa kabisa,” alisema Nditiye.

Pamoja na maelezo hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, aliwatoa hofu wananchi kwa kusema   watakaoshindwa kusajili laini zao kwa sababu ya kukosa vitambulisho vya taifa, wataandaliwa utaratibu mwingine wa kutumia simu zao.

”Malengo ya NIDA ni kusajili Watanzania milioni 25, lakini hadi sasa ni Watanzania zaidi ya milioni 16 waliosajiliwa.

”Lakini, baada ya TCRA kusema wanataka kuwa na usajili mpya wa laini za simu kwa kutumia vidole, tukasema wale wenye namba za vitambulisho vya NIDA wakitaka kusajili laini zao, watatumia vitambulisho vyao na wale wasiokuwa navyo japokuwa wameshajisajili, watatumia namba za usajili zinaitwa NIN.

”Kwa kuwa bado usajili unaendelea, basi Watanzania wasiwe na wasiwasi, kwa sababu muda wa usajili utakapokwisha wakati baadhi ya watu hawajasajili laini zao hata kama wameshajiandikisha NIDA, tutaangalia namna ya kufanya kwa sababu hilo siyo kosa lao,” alisema Kangi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,905FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles