23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YADAI UPELELEZI KESI YA ESCROW HAUJAKAMILIKA

PATRICIA KIMELEMETA NA MANENO SELANYIKA


WAKILI wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mmiliki wa Kampuni ya IPTL, Harbinder Sethi na mfanyabiashara maarufu hapa nchini, James Rugemalira, haujakamilika.

Swai alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 16, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Kwa pamoja, Sethi na Rugemalira, wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kuisababisha Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 300.

Katika hatua nyingine, upande wa utetezi katika kesi inayomkabili aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitilya na wenzake umewataka upande wa Jamhuri kufuta mashtaka ya utakatishaji fedha ili wateja wao wapate dhamana.

Mbali na Kitilya, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Miss Tanzania (1996), Shose Sinare na Ofisa wa Benki ya Stanbic, Sioi Sumari.

Kesi hiyo ilitajwa jana katika Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa na upande wa mashtaka ulisimamiwa na Wakili Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi na ule wa utetezi uliwakilishwa na Mawakili wawili, Majura Magafu na Alex Mgongolwa.

Wakili Kishenyi aliomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa sababu upelelezi haujakamilika na iliahirishwa hadi Machi 16, mwaka huu.

Magafu alidai kuwa kama upande wa mashtaka hawajakamilisha upelelezi basi liwe ni ahirisho la mwisho na pia katika  upelelezi waondoe shaka ya utakatishaji wa fedha ili washtakiwa waweze kupata dhamana kwa kuwa wamekaa mahabusu kwa muda mrefu.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa mashtaka yanayowakabili washtakiwa hayana kikomo na bado wanafanya juhudi za kuharakisha huo upelelezi.

Baada ya kutolewa kwa hoja hizo, Hakimu Nongwa aliiahirisha kesi hiyo kwa ajili ya kutajwa na kuutaka upande wa mashtaka kufanya linalowezekana upelelezi ukamilike kwa kuwa washtakiwa wapo mahabusu kwa kipindi kirefu.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi, 2013 na Septemba, 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa dola milioni 550 kwa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard nchini Uingereza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles