Na MWANDISHI WETU-DODOMA
SERIKALI imesema imegundua mchezo mchafu unaofanywa na wafanyabiashara haramu, wakiwamo majangili wanaotakatisha fedha kwa kununua mifugo mingi.
Pia, Serikali imesema imegundua imekuwa ikichungwa katika maeneo ya hifadhi za Taifa kabla haijauzwa kwenye minada.
Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alipokuwa akizungumza na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke, ofisini kwake mjini Dodoma.
Ili kukabiliana na tabia hiyo, Profesa Maghembe alisema Serikali inajipanga kushughulika na wahalifu hao.
Kwa mujibu wa Profesa Maghembe, tabia hiyo imesababisha maeneo mengi kukumbwa na migogoro mikubwa ya ardhi kwa kuwa mifugo hiyo inaharibu maeneo ya hifadhi na vyanzo vya maji.
“Tumegundua kuna genge la watakatisha fedha haramu, wananunua mifugo kwa wingi kisha wanawapa watu wawachungie maeneo yetu ya hifadhi, baada ya miezi kama sita hivi, wanakuja kuichukua na kuiuza kwenye minada kwa faida kubwa, tutashughulika nao ipasavyo.
“Wanapoingiza mifugo ndani ya hifadhi, huingia na majangili na wachoma mkaa, tumebaini karibu nusu ya mkaa unaovunwa Tanzania, huuzwa nje ya nchi. Hatutakubali vitendo hivi viendelee, ni lazima misitu yetu iliyobaki ilindwe na iendelee kuwapo,” alisema Profesa Maghembe.
Kuhusu athari za mazingira zitokanazo na uharibifu wa misitu, Profesa Maghembe alisema maeneo mengi yaliyokuwa yakipata mvua kwa miezi mitano mfululizo, sasa yamekuwa yakipata chini ya kiwango na kufikia miezi mitatu hadi miwili, hali inayotishia nchi kuwa jangwa.
Kwa upande wake, Balozi Cooke alimhakikishia Profesa Maghembe kuwa atakuwa balozi mzuri wa vivutio vya Tanzania nchini Uingereza na kuendeleza ushirikiano mzuri uliopo baina ya nchi hizo.