Na Sheila Katikula, Mwanza
Serikali imewahakikishia wahitimu wa vyuo vya elimu nchini kuwa inaendelea kuweka mazingira na sera rafiki kuwawezesha kujiajiri kwenye sekta binafsi na Taasisi za umma.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mwanaidi Ally Hamis wakati wa mahafari ya 38 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini yaliyofanyika kwa Mara ya nane ya katika kituo cha Mafunzo kanda ya Ziwa jijini hapa.
Mwanaidi alisema miongoni mwa sera ambayo tayari inatekelezwa hadi sasa ni fursa ya mikopo ya fedha inayotolewa kwenye Halmashauri hapa nchini kwa makundi ya wanawake na vijana na Walemavu ambapo wahitimu wa vyuo wanaweza kutumia kupata fedha za kujiajiri.
Aliongeza kuwa bidii na kujituma ni nyenzo muhimu itakayowawezesha kumudu maisha yao kwa kutumia elimu waliyoipata darasani na nje ya mafunzo kwani pesa siyo mtaji pekee unaoweza kumfanya mtu kujiajiri.
“Ujuzi mlioupata mkautumie kutafuta ufumbuzi wa matatizo mbalimbali hapa nchini, hivyo changamkieni fursa ya kuanzisha viwanda ili kuinua vipato vyenu,” alisema Mwanaidi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa, Prof. Juvenal Nkonoki alisema kwa mwaka wa masomo 2019/2020, jumla ya wanachuo 1412 wakiwemo wakike 861 ambayo ni asilimia 61 na wakiume 551 asilimia 39 wamefuzu na kupata astashahada ya msingi ya Mipango ya Maendeleo Vijijini.
Prof. Nkonoki alisema jumla ya wanachuo 695 wakiwemo wanaume 262 ambayo ni asilimia 37.7 na Wanawake 433 ambayo ni asilimia 62.3 wamefuzu astashahada ya Mipango ya Maendeleo Vijijini.
Aliongeza kuwa kwa upande wa Stashahada walifuzu wanachuo 428 wanaume 176 asilimia 41.1 na wakike 252 asilimia 28.9 na vile vile wanachuo 36,ambao wakiume 20 asilimia 55.6 na wakike 16 asilimia 44.4 wamepata shahada ya kwanzaya Maendeleo Mikoani.
Aidha Mkuu wa chuo hicho kanda ya Ziwa, Prof. Hozen Mayaya alisema katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 2571 wakiwemo wakiume 1009 na wanawake 1562 wametunukiwa tuzo zao katika programu nne tofauti.