Na Clara Matimo, Mwanza
Serikali imeviagiza viwanda vyote nchini kutumia teknolojia ya kisasa inayodhibiti kelele na moshi ili kuepuka uchafuzi wa mazingira, athari kwa wananchi na watu wanaofanya kazi kwenye viwanda hivyo.
Agizo hilo lilitolewa Februari 23, 2023 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Khamis baada ya kutembelea na kukagua viwanda mbalimbali Mkoani Mwanza.
Akiwa katika kiwanda cha Ziwa Steel and Wire Product ambacho uwekezaji wake umegharimu zaidi ya Sh bilioni 20 kinachozalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo nondo, mabati na misumari kilichopo Wilaya ya magu Mkoani Mwanza, Khamisi alisema kila mwekezaji anawajibu wa kuwalinda wafanyakazi wake pamoja na wananchi dhidi ya moshi maana baadhi ya watu wanaofanya kazi viwandani wamekuwa wakiathirika na moshi unaotoka wanapokuwa viwandani wakitimiza majukumu yao.
“Tuwalinde wafanyakazi na zile sumu ambazo zinatoka wakati wanafanya kazi na kuwaathiri pia tuwalinde wananchi ambao wanaishi jirani na viwanda maana moshi ukitoka nje ya kiwanda wakauvuta na unakuwa umechanganywa na kemikali si salama kwa afya zao hata hivyo naupongeza sana uongozi wa kiwanda hiki maana mmefunga mashine za kisasa ambazo zitadhibiti moshi na kelele hongereni sana,”amesema na kuongeza:
“Wafanyakazi wengi wa viwandani wamekuwa wakiumia kutokana na kutofahamu kutumia vizuri mashine zilizopo viwandani wafundisheni ili waelewe zisije zikawadhuru ili kuepuka ajari kazini zinazoweza kuzuilika pia mnapofunga teknolojia mpya hakikisheni mnawashirikisha wafanyakazi ambao ni wazawa tunahitaji nao waelewe teknolojia hizo ili kulisaidia taifa maana hakuna mtanzania aliyevumbua kompyuta au simu lakini tunao mafundi kwa kuwa walishirikishwa kwa kupewa elimu.
“Nawapongeza sana kwa uwekezaji mkubwa mliowekeza hapa sasa tunakwenda kutengeneza mazingira ya kutokukosa bidaa muhimu tunazozihitaji maana watu wanajenga kila siku na bidhaa zenu zitahitajika, endeleeni na uwekezaji serikali tutaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wa viwanda, lengo na madhumuni tukuze uchumi wetu,” amesisitiza Naibu Waziri Khamis.
Mkuu wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Rachel Kasanda amemshukuru mwekezaji kwa kuwekeza katika wilaya hiyo maana kiwanda hicho kitakuza uchumi kwa kuwa watu kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwemo Uganda, Rwanda, Kenya na Burundi wataenda ili kununua bidhaa zinazozalishwa hapo pamoja na kutoa ajira kwa vijana.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa kiwanda cha Ziwa Steel and Wire Product, Manyama Yohana alisema ziara ya Naibu Waziri Khamis kiwandani hapo imewaongezea elimu bora zaidi juu ya utunzaji wa mazingira na uhusiano baina yao pamoja na Serikali na kubainishwa kwamba ujenzi wa kiwanda hicho ulianza mwaka 2021 unatarajia kukamilika Aprili hadi Juni mwaka huu 2023 na kuanza uzalishaji kikiwa kimelenga kuanza kutoa ajira kwa wafanyakazi 1,000.
“Mkakati wa kiwanda hiki ni kuhakikisha tunahifadhi mazingira hakuna maji ambayo yatatiririka kwenda kwenye makazi ya wananchi wala hawataathiriwa na moshi maana tumefunga mashine za kisasa zinazodhibiti moshi, eneo hili litakuwa kijani sana kwa sababu tumeweka bustani maalumu ambazo tutapanda nyasi pia tumeishaanza kupanda miti ndani na nje ya kiwanda,”alieleza Yohana na kufafanua kwamba wako tayari kufuata sheria na kanuni zote zilizowekwa na serikali katika kuhifadhi mazingira.