24 C
Dar es Salaam
Thursday, July 25, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaagiza mifugo kutolewa hifadhini

Prof. Jumanne MaghembeNa Mwandishi Wetu, Geita

SERIKALI imeagiza mifugo yote ambayo ni ya raia wa kigeni kutoka nchi jirani na ile ya wazawa kutolewa haraka katika mapori ya akiba na hifadhi za misitu.

Kauli hiyo, imetolewa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe wakati wa ziara ya kikazi wilayani Bukombe mkoani Geita.

Alisema mifugo yote ya wazawa, inatakiwa pia kutolewa katika mapori ya akiba na hifadhi za misitu kwa hiari na ifikapo Juni 15, mwaka huu kusiwepo na mifugo ndani ya hifadhi.

Alisema mifugo  itakayobaki katika hifadhi hizo, itakuwa imevunja sheria na wahusika watashtakiwa na  mali zao zote zitaifishwa. “Doria ziendelee ili kuhakikisha  maelekezo haya yanatekelezwa ipasavyo,” alisema.

Kuhusu ng’ombe 454 waliokamatwa  na kuzuiliwa hifadhini, Waziri Maghembe alisema kesi yake inaendelea na kuwa suala hilo litasimamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali mstaafu, Ezekiel Kyunga.

Alisema operesheni  za kuondoa mifugo na makazi ndani ya mapori ya akiba na hifadhi za misitu, zifanyike kwa kushirikisha kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya husika ili kuondoa malalamiko ya  viongozi kula rushwa na kunyanyasa wananchi.

Alisema kuna changamoto kubwa zinazoathiri ustawi wa maliasili katika  maeneo yaliyohifadhiwa, kuwa ni ujangili na ulishaji wa mifugo.

Akitoa mfano, alisema katika pori la akiba la Moyowosi/Kigosi peke yake, kuna zaidi ya ng’ombe milioni  mbili ambao wamesababisha uharibifu mkubwa unaofikia asilimia 30 ya vyanzo vya Mto Malagarasi, ambacho ndiyo chanzo kikubwa cha maji cha Ziwa Tanganyika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles