Na Ramadhan Hassan,Dodoma
SERIKALI kwa kushirikiana na Benki ya Dunia inatarajia kuanza kutekeleza mradi wa “Tanzania ya Kidigitali” utakao gharimu zaidi ya Sh bilioni 349.
Hatua hii imekuja mara baada ya benki hiyo kuridhishwa na maandalizi ya mradi huo ambao unatazamiwa kuboresha minara ya simu 488 yenye uwezo wa 4G kutoka 2G na kujenga zaidi ya minara mingine mipya 300 itajengwa lengo likiwa ni kuimarisha huduma ya mawasilian hapa nchini.
Hayo yameelezwa leo Jumatatu Novemba 8, 2021 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk.Zainab Chaula wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya ujumbe wa benki ya dunia ulipotembelea Wizarani hapo kujionea maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo uliosainiwa Agosti 19, mwaka huu.
Dk.Chaula amesema kuwa mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa uboreshaji miundombinu ya TEHAMA Serikalini, miundombinu ya Taifa ya anuani na makazi ,maendeleo ya vijana ,biashara mtandao,uunganishaji wa mitambo ya vijijini na uchumi wa kidigitali.
“Mradi huu pia utarahisisha miundombinu na mifumo ya vituo vya huduma ya pamoja,kujenga uwezo wa ujuzi wa TEHAMA, uhamasishaji wa umma kwa ujumla pamoja na kujenga kituo cha kuendeleza na kutoa mafunzo kwa wanataaluma wa Tehama,”amesema.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Kundo Methew amesema kuwa uanzishwaji wa mradi huo unaendana na sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 ambayo inasisitiza jukumu la Teknolojia ya mawasiliano katika kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kwamba jambo hilo litapunguza pengo la kidigitali na kuleta manufaa ya mageuzi ya kidigitali nchini na kimataifa.
Kwa upande wake kiongozi wa timu na mkuu wa msafara wa Benki ya Dunia, Dk.Tim Kelly amesema wamefikia hatua hiyo kwa kuamini kuwa itasidia kuleta maendelo kwa watanzania hasa kwa kuwa wanaamini kuwa mapinduzi ya uchumi wowote duniani yanaletwa na TEHAMA.
Amesema ,ili kuwezesha uchumi jumuishi na wenye muingiliano sahihi Benki hiyo inatekeleza mradi huo kwa matamanio makubwa ya kupata matokeo chanya nakuongeza kuwa ikiwa hautafanikiwa italeta picha mbaya kwa benki hiyo.
“Kwa nafasi ya kimkakati iliyonayo Tanzania tunaamini kuwa na manufaa zaidi wa jamii nzima ikiwa ni pamoja na nchi jirani kwa kurahisisha muingiliano wa kimataifa katika biashara na masuala mengine ya mahusiano ya kijamii,”alifafanua Dk.Kelly.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo, Honest Njau amesema mradi huo ni wa miaka mitano ambapo utekelezaji wake utafanyika katika taasisi mbalimbali na utahusisha kuwajengea uwezo wataalamu ma masuala ya tehema hapa nchini.
Njau ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo utaongoza nchi kutumia uwezo wake wa kidigitali na kuhakikisha wananchi na wafanyabiashara wanapata maunganisho yenye ubora wa hali ya juu na kwa gharama nafuu.
“Huduma za umma zitapatikana kwa urahisi na kwa usalama mtandaoni na hivyo kutimiza dhamira ya kujenga uchumi imara na wa kidijitali,”amesema.