30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali: Watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano wasajiliwe

*Yazindua Mpango wa usajili wa watoto wa umri chini ya miaka mitano katika mkoa wa Tabora

*Watoto 500,000 kusajiliwa Tabora

Na Faraja Masinde, Tabora

SERIKALI imeagiza kusajiliwa kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano na kwamba huduma hiyo inatolewa bure.

Wito huo umetolewa Juni 3, 2022 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo wakati akizindua Mpango wa usajili wa watoto wa umri chini ya miaka mitano katika mkoa wa Tabora, ambapo hadi sasa Mikoa 22 nchini imenufaika na mpango huo tangu ulipozinduliwa nchini mwaka 2013.

Tunazindua

Mpango huo unatekelezwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Maendeleo una lengo la kuboresha hali ya usajili wa vizazi nchini.

Mbali na kufungua mlango wa haki ya kutambuliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, mpango huo umekuwa na matokeo makubwa ya utatuzi wa changamoto mbalimbali zilizokuwa zinaikabili Serikali na wananchi kuhusiana na usajili wa vizazi.

“Lazima tutambue kuwa cheti cha kuzaliwa ni haki ya kila mtoto aliyezaliwa katika ardhi ya Tanzania awe raia na asiye raia, kinachotakiwa ni wazazi wa mtoto husika kuthibitisha uraia wao kabla taratibu za kumsajili mtoto hazijaanza.

“Hivyo niwatake wananchi kutoa msaada na ushirikiano katika zoezi la utambuzi wa wazazi wenye sifa za kusajili watoto wenu ili wapewe vyeti vya kuzaliwa,” amesema Makondo.

Aidha, katika hatua nyingine serikali imeipongeza RITA, Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Mikoa yote ambayo Mpango huo unatekelezwa kwa namna wanavyoratibu zoezi hili kwa ufanisi mkubwa.

Kwa kutambua mchango mkubwa wa Wadau wa Maendeleo katika utekelezaji wa mpango huo, Makondo ameshukuru Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF) na Serikali ya Canada kwa namna walivyojitoa katika kuhakikisha kuwa mpango huo unafanikiwa hapa nchini.

Aidha, ameshukuru Kampuni ya Mawasiliano ya TIGO pamoja na wadau wengine kwa kuendelea kuwa sehemu ya utekelezaji wa mpango huu muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.

Kuhusu Watendaji wa Kata na Wasajili katika Vituo vya Afya, Makondo amewaagiza kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na uzalendo wa hali ya juu. Serikali haitamfumbia macho yeyote atakayekiuka taratibu na kukwamisha Mpango huo,”amesema Makondo.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Angela Anatory akizungumza kuhusu Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri Chini ya Miaka Mitano katika mkoa wa Tabora amesema lengo lake ni kuhakikisha kila mtoto ambae hajasajiliwa, anasajiliwa na kupata cheti cha kuzaliwa.

Kabidhi Wasii Mkuu, Angela Anatory akitoa maelezo kuhusu Mpango wa Usajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wa umri wa chini ya miaka mitano ambao umezinduliwa Juni 03, 2022 mkoani Tabora.

Aidha, amesema mpango huo utahakikisha kwamba kila mtoto atakayezaliwa kuanzia siku Mpango huo umeanza kutekelezwa anasajiliwa ndani ya muda mfupi baada ya tukio la kizazi kutokea.

“Chimbuko la mpango huu ni uwepo wa kiwango kidogo cha wananchi ambao wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa hapa nchini kutokana na sababu mbalimbali zilizosababisha wananchi kushindwa kusajili vizazi hivyo basi serikali na wadau kuamua kubuni Mpango huu unaoenda kutatua changamoto zilizopo katika mfumo wa awali.

“Mpango wa Usajili wa Watoto unaleta maboresho yafuatayo katika Mfumo wa Usajili; moja, kusogeza huduma za usajili karibu na maeneo ya makazi ya wananchi na huduma kupatikana katika vituo vya Tiba vinavyotoa huduma ya Mama na Mtoto na katika Ofisi za Watendaji Kata.

“Pili, kuondoa ada ya cheti kwa watoto wanaosajiliwa kupitia Mpango huu hivyo nyaraka hiyo kutolewa BILA MALIPO. Tatu, kuimarisha mfumo wa kutuma na kuhifadhi taarifa za waliosajiliwa kwa kutumia TEHAMA ambapo simu ya kiganjani iliyowekwa programu maalum hutumika,” amesema Anatory.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo(kushoto), akifurahia jambo na Kabidhi Wasii Mkuu, Angela Anatory(kulia) wakati wa kuzindua Mpango wa usajili wa watoto wa umri chini ya miaka mitano mkoani Tabora Juni 3,2022.

Kwa muji wa Anatory, mpango huo mpaka sasa umeanza kutekelezwa katika mikoa 22 ya Mwanza, Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe, Geita, Shinyanga, Lindi, Mtwara, Simiyu, Morogoro, Pwani, Mara, Dodoma, Singida, Ruvuma, Arusha, Manyara, Tanga, Kilimanjaro, Rukwa na Katavi.

“Kwa ujumla Mafanikio ya utekelezaji wa Mpango huu katika mikoa iliyotangulia ni makubwa na mpaka sasa zaidi ya watoto 7,549,878 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa,hivyo kuongeza kiwango cha usajili kutoka asilimia 13 mwaka 2012 na kufikia asilimia 65 mwaka 2021.

“Hii ni sawa na kusema kwamba zaidi ya nusu ya watoto nchini wamepata haki yao ya msingi ya kutambuliwa na taarifa zao kuingizwa katika mfumo rasmi wa utambuzi wa serikali,” amesema Anatory.

Kuhusu mkoa wa Tabora, amesema kutakuwa na awamu mbili za utekelezaji ambapo ya kwanza ambayo imeanza Juni 3, 2022 ikiwa ni kampeni ya wiki mbili kwa ajili ya kuwasajili na kuondoa bakaa ya watoto wote wa umri chini ya miaka mitano wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa.

“Awamu ya pili itahusisha kuusimika mfumo katika vituo hivyo ili kuendelea kutoa huduma kwa watoto wanaozaliwa ili kuepuka kutengeneza bakaa kwa mara nyingine.

“Kila kituo cha Usajili kina wahudumu wasiopungua wawili waliopata mafunzo ya kina ya usajili ili kuhakikisha muendelezo wa upatikanaji huduma mara ikitokea mmojawapo amesafiri au ana majukumu mengine,” amesema Anatory.

Katika hatua nyingine, Anatory ameongeza kuwa ili kuhakikisha kwamba Mpango unatekelezwa kikamilifu, wamefanya vikao na mafunzo mbalimbali katika ngazi tofauti ikiwa ni pamoja na viongozi na wasajili wasaidizi kwa lengo la kuongeza uelewa wao kuhusu masuala ya Usajili wa Vizazi.

“Mkoa wa Tabora una changamoto ya kuwa na muingiliano wa raia wa nchi jirani ambao inawezekana wengine walikuja na watoto wa umri chini ya miaka 5 ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo, Sura ya 108, watoto hao hawastahili kusajiliwa kwani wamezaliwa nje ya mipaka ya Tanzania,” amesema Anatory.

Mwakilishi wa Shirika la kuhudumia Watoto Duniani (UNICEEF), Shalin Bahuguna akieleza ushirikiano uliopo baina ya Serikali ya Tanzania katika kuboresha kwa kuwezesha kusogeza huduma karibu na wananchi na hiyo ni pamoja na mpango wa usajili wa kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.

Ikumbukwe kuwa, tangu kuanza kwa usanifu wa mfumo bunifu wa usajili wa vizazi, UNICEF imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Serikali katika kuutekeleza kwa ukamilifu, mkoa mmoja baada ya mwingine, kwa lengo la kuifikia nchi nzima.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania, Shalini Bahunguna amesisitiza dhamira ya UNICEF kwa Serikali na kutambua msaada mkubwa kutoka kwa Serikali ya Canada na TIGO katika kufanikisha mpango huo muhimu unaolenga kusajili watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano na kuwapatia cheti cha kuzaliwa kama moja ya haki za msingi.

“Haki ya kusajiliwa baada ya kuzaliwa imeainishwa katika Mkataba wa Haki za Mtoto, na tunapongeza maendeleo ya Tanzania kuhakikisha haki hii inapatikana kwa kila mtoto,” amesema Bahuguna.

Aidha, ametoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa mfumo wa usajili wa vizazi unapangwa na kufadhiliwa katika ngazi ya taifa, mikoa na wilaya na kuhimiza kuwa uandikishaji wa raia unaunganishwa katika kazi za kawaida za halmashauri za wilaya na mikoa ili kuendeleza mafanikio makubwa katika mfumo huu wa kitaifa,” amesema Bahuguna.

Upande wake Mkurugenzi Mwandamizi na Mkuu wa Ushirikiano, Kamisheni Kuu ya Canada, Helen Fytche akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi mjini Tabora amesema kuwa nchi hiyo inahakikisha upatikanaji wa huduma na haki muhimu, hasa kwa wanawake na wasichana.

Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Canada, Helen Fytche akitoa ufafanuzi jinsi Serikali yake kupitia shirika hilo linavyoendelea kuisaidia Tanzania katika uboreshaji wa huduma za kijamii.

“Ni kipaumbele kwa Canada chini ya sera yake ya Kimataifa, ya Usaidizi wa Wanawake, kwani inachangia katika kutokomeza umaskini na kujenga dunia yenye amani zaidi, jumuishi zaidi na yenye ustawi zaidi.

“Canada inajivunia kutoa zaidi ya dola za Canada milioni 30 kwa ajili ya kusaidia mfumo wa usajili wa watoto wa chini ya miaka mitano wa Tanzania ambao unaondoa vikwazo vya upatikanaji kati ya mijini na vijijini, matajiri na maskini, na wavulana na wasichana.

“Mradi huu ni mfano bora wa ushirikiano wa kibunifu – Serikali ya Tanzania, sekta binafsi na washirika wa maendeleo wameungana kubuni na kuzindua mchakato wa ubunifu wa usajili wa vizazi vya watoto zaidi ya milioni 7.5 tangu 2013,” amesema Fytche.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles