RAMADHAN HASSAN-DODOMA
SERIKALI imesema walimu hawapaswi kudai mbalimbikizo ya nyongeza ya mwaka ya mshahara kwa miaka ambayo nyongeza hiyo haikutolewa.
Hayo yalielezwa jana bungeni na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Zainab Musa Bakar (Chadema).
Katika swali lake, Zainab alidai walimu wote nchini wameingia katika mkataba na mwajiri wake ambao pamoja na mambo mengine unaonesha uwepo wa ‘increment’ kila ifikapo Julai.
Mbunge huyo alidai tangu iingie madarakani, Serikali ya Awamu ya Tano haijawapa walimu stahiki hiyo.
“Je, walimu watalipwa hiyo kama malimbikizo au hiyo imeshapotea?” aliuliza mbunge huyo.
Akijibu, Naibu Waziri Waitara, alisema Serikali imekuwa ikitekeleza miongozo mbalimbali iliyowekwa kuhusu masilahi ya walimu ikiwa ni pamoja na kutoa nyongeza za mwaka za mishahara kulingana na utendaji kazi mzuri wa kazi na kwa kuzingatia tathmini ya utendaji kazi ya kila mwaka.
“Kwa mujibu wa kanuni E.9 (1) ya kanuni za kudumu katika utumishi wa umma za mwaka 2009 toleo la tatu, nyongeza ya mwaka ya mishahara haipaswi kuombwa au kudaiwa na walimu bali Serikali ndiyo yenye uamuzi wa kutoa au kutotoa nyongeza hiyo kutokana na sera za kibajeti kwa mwaka husika,” alisema Waitara.
Waitara alisema watumishi wa umma wakiwemo walimu wanastahili kupewa nyongeza ya mwaka ya mshahara iwapo bajeti ya mishahara inaruhusu.
“Kutokana na ufinyu wa bajeti, nyongeza hiyo haikutolewa kwa watumishi kwa mwaka wa fedha wa 2003-2004, 2004-2005, 2008-2009, 2011-2012,2012-2013, na 2016-2017.
“Hata hivyo, kwa kutambua utendaji kazi mzuri, Serikali ya awamu ya tano, ilitoa nyongeza ya mwaka ya mshahara kwa watumishi wote wakiwemo walimu katika mwaka wa 2017-2018,” alisema.
Waitara alisema, Serikali itaendelea kutoa nyongeza ya mwaka ya mshahara kwa watumishi wote kadiri uwezo wa kulipa utakavyoruhusu.
Pamoja na hayo, Waitara alisisitiza walimu hawapaswi kudai malimbikizo ya nyongeza ya mwaka ya mshahara kwa miaka ambayo nyongeza hiyo haikutolewa.