33.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 19, 2021

Serikali: Viwanda vipya 8,477 vimeanzishwa

NA RAMADHAN HASSAN –Dodoma

SERIKALI imesema tangu Awamu ya Tano iingie madarakani, viwanda 8,477 vimeanzishwa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara na kati ya hivyo, vikubwa ni 201, vya kati ni 460 vidogo ni 3,406 na vidogo sana ni 4,410.

Hayo yalielezwa jana bungeni na Wizara ya Viwanda na Biashara wakati ikijibu swali la Mbunge wa Mbulu Mjini, Zacharia Issaay (CCM).

Katika swali lake, Issay alihoji ni lini Serikali itaanza kufanya tathmini ya mafanikio ya viwanda 100 kwa kila wilaya ili kuchochea uchumi wa nchi.

Ikijibu swali hilo, Wizara ya Viwanda na Biashara ilieleza kuwa Serikali ilifanya tathmini ya jumla ya upimaji wa mafanikio ya azma ya ujenzi wa viwanda Februari, mwaka huu ambayo ilionyesha jumla ya viwanda 8,477 vimeanzishwa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani.

Vilevile wizara ilisema kuwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, imeandaa mpango mahsusi wa kufanya tathmini pana ya viwanda vyote vilivyopo Tanzania Bara mwaka 2020/2021 kupitia mpango maalumu unaojulikana kama Industrial Mapping.

Ilieleza kuwa mpango huo utazingatia pia kufanya tathimini ya mpango wa viwanda 100 kila mkoa na utabainisha idadi na aina ya viwanda vilivyopo nchini, ajira, bidhaa zinazozalishwa, mapato, teknolojia zinazohitajika pamoja na malighafi zinazotumika ili uanzishwaji wa viwanda uendane pia na malighafi zinazopatikana hapa nchini ili kuwa na viwanda endelevu.

Aidha, wizara hiyo ilieleza kuwa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na sekta binafsi, inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuendeleza ujenzi wa viwanda ili azma ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaojengwa kupitia viwanda, iweze kufanikiwa ifikapo mwaka 2025.

Pia, wizara hiyo iliweka kumbukumbu sahihi kwamba Ofisi ya Rais Tamisemi kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara ilianzisha kampeni mahsusi yenye lengo la kufanikisha ujenzi wa viwanda vipya 100 kwa kila mkoa ili kuunga mkono azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, na si viwanda 100 kwa kila wilaya kama swali la msingi lilivyouliza.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
156,882FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles