23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI UINGEREZA YASHINDWA KESI YA BREXIT

LONDON, UINGEREZA

MAHAKAMA ya Juu nchini Uingereza imesema Waziri Mkuu Theresa May lazima apate idhini ya Bunge kabla ya kuanzisha mchakato wa nchi hiyo kujiondoa Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit.

“Leo (jana) kwa wingi wa majaji wanane dhidi ya watatu, mahakama inahukumu kuwa Serikali haiwezi kuanzisha kipengele cha 50 kama inavyotaka bila sheria ya Bunge inayoiruhusu kufanya hivyo,” alisema Jaji David Neuberger wakati akisoma hukumu hiyo.

Katika hukumu hiyo, mahakama ilisema muswada kama huo ambao unatarajiwa kupelekwa bungeni ama baadae wiki hii au wiki ijayo, unaweza kuwa mkataba mfupi sana.

Mara baada ya kutolewa hukumu hiyo, waziri anayehusika na Brexit, David Davis, alisema Serikali itawasilisha sheria ya waziwazi ndani ya siku chache kutaka idhini ya Bunge kuanzisha mchakato huo.

“Tutawasilisha ndani ya siku chache zijazo muswada wa sheria kuipa Serikali mamlaka ya kisheria ya kuanzisha kipengele cha 50 na kuanza mchakato rasmi wa kujiondoa,” alisema Davis na kuongeza kuwa huu ndiyo utakuwa muswada wa wazi zaidi iwezekanavyo kutekeleza uamuzi wa watu na kuheshimu hukumu ya Mahakama ya Juu.

mwanaharakati Gine Miller ndiye aliyefungua shauri hilo mahakamani, akitaka Bunge liwe na usemi katika kuanzisha mchakato wa Brexit.

Wakati wa kura za maoni kuhusu kujiondoa Umoja wa Ulaya, wabunge wengi walipiga kura kutaka Uingereza ibakie katika chombo hicho.

Hata hivyo, chama kikuu cha upinzani cha Labour, kilisema hakitazuia Brexit ingawa kitajaribu kuifanyia marekebisho sheria hiyo.

Taarifa za vyombo vya habari zimesema wabunge 80 wa Labour kati ya 650 katika Bunge la Uingereza watapuuza msimamo wa Kiongozi wa chama chao, Jeremy Corbyn, na kupiga kura kupinga kuanzisha mchakato huo.

Aidha chama kidogo cha Liberal Democratic kimesema kitapinga mchakato mzima wa Brexit isipokuwa iitishwe kura ya pili ya maoni kuhusu makubaliano ya mwisho.

Wakati huo huo, Waziri Kiongozi wa Scotland, Nicolas Sturgeon ameibua uwezekano wa kura nyingine ya kutaka uhuru wa Scotland baada ya mahakama hiyo kuamua kwamba Bunge la Scotland halihitaji kushauriwa kuhusu kuanzisha mchakato wa Brexit.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles