24.6 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI TAWASAKA WAUAJI WA KINARA VITA YA UJANGILI

Na LEONARD MANG’OHA

-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, amethibitisha kuuawa mwanaharakati wa kupinga ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo wa Taasisi ya Pams Foundation ya Arusha, Wayne Lotter (51), kwa kupigwa risasi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Profesa Maghembe alisema hadi sasa hawajafanikiwa kufahamu lengo la watekelezaji wa mauaji hayo.

“Nitoe pole kwa familia na nchi yake kwa sababu amekuwa akipigana vita kubwa ya kupinga ujangili, hatujui lengo la mauaji yake, polisi wanaendelea kufuatilia kubaini waliotekeleza tukio hilo ili waweze kukamatwa,” alisema Profesa Maghembe.

Lotter alikuwa Mkurugenzi na Mwanzilishi Taasisi isiyo ya kiserikali ya Pams Foundation, inayojihusisha na kulinda na kupambana na mauaji ya tembo barani Afrika.

Inaelezwa tangu mwaka 2012 aliwezesha jumla ya wawindaji 2,000 wa tembo na wasafirishaji wa meno ya tembo kukamatwa, huku akidaiwa kusaidia kupunguza mauaji ya wanyama hao kwa karibu asilimia 50.

Taarifa za kuuawa kwa Lotter zilianza kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii tangu juzi, zikieleza kuwa aliuawa Jumatano jioni Agosti 16, mwaka huu.

Waziri Maghembe hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa undani, zaidi ya kusisitiza tu kwamba vyombo vya dola vilikuwa vikilifuatilia kwa ukaribu tukio hilo.

Kumekuwa na taarifa za kukanganya juu ya mahali alikouawa Lotter, wakati nyingine zikidai kuwa aliuawa karibu na shule ya IST iliyopo Masaki, jijini Dar es Salaam, nyingine zilieleza kuwa aliuawa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA).

Hakuna chombo chochote cha Serikali kilichokuwa tayari kuthibitisha mahali ambako Lotter aliuawa, ingawa taasisi ya Pams aliyokuwa akiiongoza katika taarifa yake ilieleza kuwa, kiongozi wao huyo aliuawa katika eneo la Masaki, jijini Dar es Salaam.

Msemaji wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Paschal Shelutete, hakuwa tayari kuzungumzia tukio hilo, zaidi akilitaka gazeti hili liwasiliane na Jeshi la Polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo, aliliambia gazeti hili kuwa, anayepaswa kulizungumzia tukio hilo ni Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Taarifa ambazo zimeripotiwa na vyombo vya habari vya kimataifa zinaeleza kuwa, Lotter aliuawa wakati akitoka Uwanja wa Ndege JNIA akielekea hotelini, ambapo gari alilokodi (tax) lilizuiwa kwa mbele na gari jingine ambalo walishuka watu wawili na kumpiga risasi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, tangu mwaka 2009, Lotter amekuwa akipokea taarifa za vitisho vya kuuawa kutoka kwa watu wasiofahamika.

Zinaelezwa kuwa, Lotter aliondoka kwa ndege kwenda Dar es Salaam bila kufahamu kuwa kulikuwa na watu waliokuwa wakimfuatilia tangu akiwa KIA.

Taarifa hizo zinadai kuwa, wauaji baada ya kutekeleza tukio hilo walichukua kompyuta mpakato (Laptop) aliyokuwa nayo.

 

Taasisi ya Pams katika taarifa yake nayo ilithibitisha taarifa za kifo hicho cha Lotter, ambaye ilimtaja kama mtu aliyetumia sehemu ya maisha yake kwa wanyama Afrika, akianza kufanya kazi kama  mwangalizi wa misitu na mbuga nchini mwake Afrika Kusini, alipokuwa kijana, kabla ya kuwa mwanaharakati wa kupambana na mauaji dhidi ya tembo.

Imemuelezea Lotter kama mtu aliyejali sana maisha ya watu na wanyama hapa duniani.

Pams imeeleza kuwa, tangu mwaka 2009 aliungana na wenzake, Krissie Clark na Ally Namangaya kuanzisha Taasisi ya Pams na kwamba wote walifanya kazi kwa kushirikiana na jamii nchini Tanzania kulinda haki za wanyama bila kuchoka.

Lotter anaelezwa kwamba aliamini jamii ndiyo mlinzi hodari wa wanyama wa Bara la Afrika.

Kupitia kazi zake katika Taasisi ya Pams, inaelezwa alisaidia kutoa mafunzo kwa maelfu ya watu kwenye vijiji mbalimbali ili kufanya doria kila kona ya Tanzania.

Katika utendaji wake wa kazi, Lotter anaelezwa alitumia mbinu za kiusalama kupambana dhidi ya mauaji ya tembo, ambayo yalifanikiwa na kusaidia kwa kiwango kikubwa kuzuia mauaji hayo.

Pams pia imeuelezea utulivu wa Lotter, uwezo mkubwa wa kiakili, tabia nzuri na mwingi wa utani, ilikuwa sifa iliyomfanya awe mtu wa kipekee kwa watu wote waliomzunguka, walifurahi na kutabasamu pamoja.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Pams, Lotter ameacha mke Inge, mabinti zao Cara Jayne na Tamsin, na wazazi wake Vera na Charles Lotter.

“Sote tunahuzunika pamoja na familia yake, marafiki zake na wafanyakazi wenzake. Urithi wake utaendelea kwa kuenzi kazi zake. Jeshi la Polisi la Tanzania limefungua jalada la upelelezi dhidi ya kifo chake,” ilieleza taarifa hiyo.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles