26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 5, 2023

Contact us: [email protected]

Serikali: Shule hazitafungwa kwa kukosa chakula

majaliwaNa Debora Sanja, Dodoma

SERIKALI imesema hakuna shule ya sekondari ya bweni nchini itakayofungwa kutokana na ukosefu wa chakula.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Kassim Majaliwa, alipojibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM).

Katika swali lake, Bulaya alitaka kujua lini Serikali italipa madeni ya wazabuni wanaosambaza chakula katika shule na taasisi za Serikali, ikiwemo Sh bilioni mbili wanazodai wazabuni kutoka Mara.

Alisema wazabuni wote wanaoidai fedha Serikali watalipwa fedha zao.

“Hata hivyo, kuanzia mwaka 2014/2015, Serikali imekuwa ikiwalipa wazabuni fedha zao kila mwezi, kwa mfano Oktoba mwaka jana tulilipa shilingi bilioni 3.5, Novemba tulilipa shilingi bilioni 2.1 na Machi mwaka huu tulilipa shilingi bilioni 8.4,” alisema Majaliwa.

Alisema haitatokea shule yoyote kufungwa kutokana na uhaba wa chakula na mkuu wa shule hana mamlaka ya kuifunga shule.

“Kama mkuu wa shule anataka kufunga shule kutokana na ukosefu wa chakula lazima awasiliane na mkurugenzi, mkurugenzi atawasiliana na katibu tawala atakayewasiliana na katibu mkuu kwa kuwa katibu mkuu ndiye mwenye mamlaka ya kutangaza kufungwa kwa shule,” alisema Majaliwa.

Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Ngara, Deogratius Ntukamazina (CCM), Majaliwa alisema mwaka 2014/2015 Serikali ilitenga Sh bilioni 42.1 kwa ajili ya huduma ya chakula cha wanafunzi wa sekondari za bweni.

“Hadi Aprili mwaka huu, shilingi bilioni 28.1 zilikuwa zimetolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Ngara ilipata shilingi milioni 171.3 kuhudumia shule za sekondari Kabanga, Lukole na Muyenzi,” alisema Majaliwa.

Alisema kuanzia Januari hadi Aprili mwaka huu, Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya chakula cha wanafunzi na kuwawezesha wazabuni.

Katika swali lake, Ntukamazina alitaka kujua lini Serikali itawalipa wazabuni wanaosambaza vyakula shuleni pamoja na kupeleka fedha katika shule za Kabanga, Muyenzi na Lukole.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles