28.3 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali Morogoro yapiga marufuku shughuli za utalii katika vyanzo vya maji

Na Ashura Kazinja, Morogoro

SERIKALI mkoani Morogoro imesitisha wananchi kufanya shughuli za Utalii katika maeneo yote ya vyanzo vya maji mkoani humo hadi pale yatakapowekwa mazingira salama kwa watu wanaotembelea maeneo hayo, baada ya kujitokeza takribani matukio matano ya vifo kwenye vyanzo hivyo.

Akizungumzia changamoto hiyo Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando, amesema  kumekuwa kukijitokeza matukio ya kufa maji katika maeneo hayo na wengine kupotea na kukosa msaada wa kuokolewa mapema na kwamba kwa kuliona hilo serikali imeamua kusitisha shughuli za utalii hadi itakapojiridhisha kuwepo kwa usalama kwenye maeneo hayo.

Msando amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya Mwanafunzi John Benako (20) wa Chuo cha Liti kilichopo katika wilaya ya Morooro baada ya kuzama na kufa maji alipoenda kuogelea kwenye mto Mambogo pamoja na wengine saba, ambapo alipotea na hakuweza kuonekana.

Ameeleza kuwa baada ya jitihada za kumtafuta toka jana usiku Mei 15, 2022 kwa kutumia jeshi la zima moto na uokoaji  kushindikana, na juhudi hizo kuendelea mpaka Mei 16, ambapo wananchi kwa kushirikiana na jeshi hilo waliweza kuupata mwili wa marehemu.

“Kifo hicho kimetokea baada ya yeye kuzama kwenye mto Morogoro toka jana alipokuwa ameenda kwenye eneo la Mambogo ambalo ni chanzo chetu cha maji akiwa na wananfunzi wenzake saba, ndipo watatu kati yao akiwemo marehemu waliingia mtoni kuogelea na mmoja kutoonekana.

“Pili ni kutoa tamko na maelekezo kwamba nimesitisha shughuli zote za utalii zinazofanyika ndani ya chanzo hicho cha maji kuanzia leo mpaka pale tutakapokaa kama kamati ya ulinzi na usalama na kutoa maelekezo tofauti ya namna gani shughuli za utalii zinaweza kufanyika kwa usalama,” alieleza Msando.

Aidha, amepiga marufuku kwa kupitia bonde la wami Ruvu kuwa ni marufuku mtu yeyote kuingia katika eneo hilo mpaka pale utakapotolewa utaratibu mzuri, na kwamba matukio ya aina hiyo yamekuwa yakijirudia na kwamba tukio hilo ni la tano na kwamba waathirika wengi ni wageni wasiojua kuwa kuna maeneo sio salama.

Aidha ametoa rai kwa wananchi kuheshimu vibao vilivyowekwa ili kutoa maelekezo katika maeneo hayo kuonyesha maeneo yasiyoingilika kwa ajili ya usalama wao, na kwamba nia ni kuwalinda wananchi na kuepuka matukio hayo ya kusikitisha.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa bodi ya Bonde la Maji wami Ruvu, Mhandisi Elibariki Mmasy,  amewataka wananchi mkoani humo kujiepusha kuendesha shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya vyanzo vya maji kwa ajili ya usalama wao na wa vyanzo hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles