28.3 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali: Milango iko wazi kwa vyombo vya habari

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Serikali imesema milango iko wazi kwa chombo chochote cha habari kinachohitaji kuungwa mkono kuhusu matayarisho au maboresho ya sera za unyanyasaji wa kijinsia ndani ya vyumba vya habari.

Aidha, imesisitiza kuwa utayari huo ni pamoja na kutafuta wataalamu wa sheria za kazi kwa ajili ya kusaidia vyombo hivyo ili kuwezesha tasnia hiyo kuwa na mazingira rafiki na kwa kila mtu.

Kaimu Mhariri Mkuu wa Gazeti la Uhuru, Jane Mihanji, akitoa mada kwenye Mjadala huo.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam Aprili 20, 2022 na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO, Rodney Thadeus wakati akihitimisha Mjadala kuhusu Sera ya Jinsia kwenye vyumba vya habari iliyoandaliwa na Shirika la Internews Tanzania ukikutanisha wadau mbalimbali wa habari.

Rodney amesema uzoefu unaonesha kuwa sheria nyingi kwenye vyombo vya habari bado haziwekwi wazi jambo ambalo linawanyima msaada walengwa.

“Sisi upande wetu kama serikali tutawasaidia kutafuta wataalamu mbalimbali wa sheria za kazi ili kutengeneza mazingira mazuri na yenye uwazi kwa wafanyakazi.

“Kwani kuendelea kuwapo kwa mazingira ya ufichwaji wa taarifa ndiko kumekuwa kukisababisha watu wanafanyiwa vitendo visivyo vya kiungwana na hawasemi kwa waajiri wao.

“Lengo letu upande wa serikali ni kuona sekta hii ya habari ikitekeleza majukumu yake vizuri, ndiyo sababu pia tumeenza kuzifanyia kazi baadhi ya sera kwa kushirikiana na wamiliki wa vyombo vya habari kwani bila kufanya hivyo baadae watu wataogopa kufanya kazi kwenye tasnia hii,” amesema Rodney.

Mhariri Mkuu Mtendaji wa Jarida la Fama, Jesse Kwayu akichangia mada kwenye mjadala huo.

Kuhusu changamoto ya unyanyasaji wa kingono katika maeneo ya kazi hasa katika vyombo vya habari inayokabiri wanawake kwa kiasi kikubwa amesema mbali na kufanyia kazi eneo la sheria pia wafanyakazi wanapaswa kujiamini ili kuondoa viashiria vya kunasa kwenye vishawishi.

“Ni kweli kuna shida ya kupata kazi lakini ni lazima mtu ahakikishe anafanya kazi kwenye mazingira bora na salama,kwani anapofanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia anapungukiwa na maadili katika uitendaji wake wa kazi.

“Hili siyo jambo la kufumbia macho kwa tasnia yetu ya habari ndio maana milango iko wazi kwa chombo chochote cha habari kinachohitaji kuungwa mkono kuhusu matayarisho au maboresho ya sera hizi,” amesema Rodney.

Awali, Mwakilishi wa Internews Tanzania, Angela Nicoara akifungua mjadala huo alisema kuwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia katika vyumba vya habari nchini havikubaliki na kamwe halipaswi kupewa nafasi.

Sehemu ya washiriki.

Upande wake, Kaimu Mhariri Mkuu wa Gazeti la Uhuru, Jane Mihanji, alisema kuwa kuna haja kubwa kwa Internews kusaidia vyumba vya habari katika kuhakikisha kuwa vinakabiliana na changamoto ya unyanyasaji wa kijinsia.

“Bado kuna changamoto kubwa ya unyanyasaji wa kingono ndani ya vyumba vya habari, kwani ni vichache tu ndio vimekuwa na miongozo ambayo nayo bado imekuwa haiwekwi bayana, hivyo inakuwa ni changamoto pindi mtu anapofanyiwa ukatili hajui aanzie wapi

“Hivyo, niombe Internews mtusaidie katika hili kwa ustawi wa tasnia ya habari kwani changamoto hii ni kubwa,” amesema Mihanji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles