Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Juni 5, mwaka huu wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yatakayofanyika kitaifa jijini Dodoma.
Sera hiyo ya mwaka 2024 inalenga kuimarisha mfumo jumuishi wa uratibu miongoni mwa wadau wanaosimamia na kutekeleza shughuli za Uchumi wa Buluu nchini pamoja na kuongeza tija ya uwekezaji unaofanyika katika rasilimali zake.
Akizungumza leo Mei 27,2024 na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk. Selemani Jafo, amesema dhana ya Uchumi wa Buluu inahusisha shughuli za kiuchumi na kijamii zinazotekelezwa katika bahari, maziwa, mito, mabwawa na maji chini ya ardhi bila kuathiri mazingira.
Kwa mujibu wa Dk. Jafo, Tanzania ina kilomita za mraba 61,500 za maeneo ya maji baridi yanayofaa kwa matumizi mbalimbali pamoja na kilomita za mraba 64,000 za maji ya kitaifa katika bahari na kilomita za mraba 223,000 za ukanda maalumu wa uchumi wa bahari. Vilevile ina kilomita 1,424 ambazo ni muhimu kwa shughuli za uvuvi, ukuzaji viumbe maji na utalii.
Waziri huyo amesema pia kabla ya kilele cha maadhimisho hayo kutakuwa na shughuli mbalimbali ambapo Mei 29,2024 watagawa hati miliki za kimila 4,450 pamoja na hati ya misitu wilayani Mpimbwe mkoani Katavi.
Ugawaji wa hati hizo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa urejeshaji uoto wa asili ambao unatekelezwa katika wilaya saba kwenye Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa na Katavi.
Amesema shughuli nyingine zitakazozinduliwa mkoani Katavi ni josho la mifugo, banio na birika la kunyweshea maji mifugo.
Waziri Jafo amesema Mei 31,2024 kutakuwa na kongamano la kitaifa la wadau wa mazingira litakalofanyika jijini Dar es Salaam lenye kaulimbiu isemayo ‘Mabadiliko ya tabianchi na athari zake’ ambapo mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.
“Wadau watapata fursa ya kujadili mada adhimu zinazohusu changamoto za hifadhi ya mazingira na kutoa mwelekeo na hatua muhimu zinazopaswa kuchukuliwa na taifa letu,” amesema Dk. Jafo.
Dk. Jafo amesema pia Juni Mosi kutakuwa na kampeni ya usafi wa mazingira kitaifa ambayo itafanyika katika Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam), Kanda ya Ziwa (Geita), Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kanda ya Magharibi (Kigoma), Kanda ya Kaskazini (Arusha) na Kanda ya Kusini (Lindi).
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo inasema ‘Urejeshwaji wa ardhi, ustahimilivu wa hali ya jangwa na ukame’.