29.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kuzibana Asasi za kiraia

*Ni baada ya kubaini kuwapo kwa udanganyifu

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Serikali imesema itaanza kutathimini utendaji kazi wa Asasi zote za kiraia nchini baada ya kubaini kuwapo kwa baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitumia fursa hiyo kujinufaisha kiuchumi.

Hayo yamebainishwa Dar es Salaam Agosti 9,2022 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Patrobas Katambi katika ufunguzi wa kongamano la siku mbili la vijana.

Katambi amesema Serikali haiwezi kufumbia macho suala hilo kwani watu wengi sikuhizi wamekuwa wajanja na wamekuwa wakitumia mbinu ya kujitangaza mbele ya jamii kwamba wanadhamira ya kusaidia vijana na kupokta misaada kutoka kwa wafadhili lakini matokeo yake imekuwa ikiwanufaisha wao binafsi kinyume na lengo lililokusudiwa.

“Lengo la Serikali ni kuona Asasi zilizojisajili kwa ajili ya kusaidia vijana zikifanya hivyo lakini hata hivyo kwa asiku za karibuni kumekuwapo na baadhi ya watu wachache wasiokuwa waaminifu ambao wamekuwa wakizitumia kujinufaisha.

“Kama Serikali tumebaini hilo, tumeanza mchakato wa kufanya tathimini ya utendaji wa Asasi zote za kiraia zilizopo nchini kujua kama kweli wanasaidia vijana au la.

“Wapo baadhi ya wajanja ambao wanadai wanasaidia vijana kumbe wanajinufaisha wenyewe kujenga majumba ya kifahari kama maghorofa,” amesema Katambi.

Aidha, Katambi amefafanua kuwa kundi la vijana ni muhimu nahivyo ndiyo sababu serikali inakuja na mkakati huo ikiwemo kubadilisha sheria na kuipa fursa sekta binafsi kukua na kuwainua vijana kiuchumi kwani ni ni sehemu muhimu katika maendeleo ya taifa.

“Pamoja na hatua hizi nzuri za kufanya mageuzi ambazo zinaendelea kuchukuliwa ni vyema pia vijana mkazingatia kujitokeza kwenye zoezi la kuhesabiwa Agosti 23, mwaka huu ili serikali ijue takwimusahihi za vijana na kuangalia namna ya kuboresha mahitaji yenu,” amesema Katambi.

Sambamba na hayo Nabu Waziri huyo pia amewataka viongozi walio kwenye nafasi hizo kutanguliza maslahi ya vijana mbele kwani ndiyo taifa la hapo baadae.

“Niwaombe wenzangu tulioko kwenye nafasi za uongozi lazima tuangalie vijana na siyo kunyanyua mabega yetu juu,” amesema Katambi na kusisitiza kuwa serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa vijana kujikwamua kiuchumi na kielimu na kwamba itaendelea kufanya hivyo.

Akizungumzia kauli hiyo ya serikali, Mwenyekiti wa Asasi hizo za Kiraia, Lilian Bondo amesema kuwa wamepewa changamoto muhimu ambayo wataijadili na wadau wote.

“Tumepokea changamoto iliyotolewa na serikali hivyo tutaifanyia tathimini pamoja na wadau wote ili kubaini ukweli wa hili lililoibuliwa,” amesema Lilian.

Akizungumzia Kongamano hilo linalofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City ikiwa ni katika kuelekea kilele cha siku ya kimataifa ya vijana Duniani Agosti 12, Mwaka huu, Mkurugenzi wa Bridge For Change, Ocheck Msuya amesema kuwa kongamano hilo limeandaliwa na vijana wenyewe kwa kushirikiana na mashirika ya vijana kutoka kada mbalimbali.

“Tumehusisha pia vijana wenye ubobevu katika nyanja tofauti baada ya kuchambua na kusoma mahitaji ya vijana katika kiwango cha kitaifa, kikanda na kimataifa. Huu ni mwanzo wa jukwaa la pamoja la uandaaji mipango, utekelezaji na nufuatiliaji wa programu na sera zinazolenga maendeleo ya vijana katika sekta binafasi na serikalini,” amesema Msuya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles