25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI KUTUMIA MAKAA YA MAWE KUZALISHA UMEME NCHINI

Na Mwandishi Wetu,

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amewahakikishia Watanzania juu ya upatikanaji wa uhakika wa nishati  ya umeme, kwani chanzo chake ni gesi asilia kwa asilimia 50 ingawa lengo la Serikali ni kufanya iwe asilimia 40 katika vyanzo vyake.

Alisema umeme unapatikana bila tabu kila mahali siku za karibuni  nchini kote kutokana na ukweli kuwa gesi asilia ndio  chanzo chake  na chenye uhakika.

Muhongo aliyasema hayo alipofungua kikao kazi cha wadau kilichofanyika katika kiwanda cha uchakataji wa gesi Madimba mkoani Mtwara, kikao ambacho kimehusisha watendaji wa wizara yake na kampuni zilizowekeza katika utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta nchini.

“Kwa sasa tunazalisha umeme wetu kwa kutumia gesi asilia ambayo imeimarisha uhakika wa upatikanaji wa umeme ukilinganisha na ilivyokuwa huko nyuma, tulipokuwa tunategemea vyanzo vya maji ambavyo vina matatizo ya kukauka kutokana na kupungua  kiasi cha mvua, lakini lengo letu ni kupunguza matumizi ya gesi katika kuzalisha umeme hadi ifikie asilimia 40 tu na hiyo itawezekana baada ya kuanza kutumia makaa ya mawe kuzalisha umeme,” alifafanua bila kusema lini umeme kutokana na makaa ya mawe utaanza kuzalishwa.

Alisema mipango ya Serikali ni kuona kunakuwa na umeme wa uhakika unaotosha kwa matumizi yote ya viwandani na majumbani ili kuharakisha kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi kuelekea  uchumi wa viwanda.

Tanzania baada ya kujenga Mtambo wa LNG, inategemea kuuza nje sehemu kubwa ya gesi yake asilia na itajenga kiwanda kikubwa cha mbolea.

Alisema ili kuhakikisha lengo la umeme wa uhakika linatimia, Serikali imeweka mikakati kadhaa ikiwa ni pamoja na kupanua njia za umeme, kuimarisha mitambo ya uzalishaji na kuboresha miundombinu ambayo imechakaa na kutumia rasilimali nyingine katika kuzalisha umeme.

Alipoulizwa swali kwanini umeme unakatika mara nyingi mkoani Mtwara na Lindi pamoja na kutumia umeme wa gesi asilia anaodai umeimarika, Muhongo alisema zipo sababu kadhaa za kiufundi zinazosababisha hali hiyo, ikiwamo njia ndogo ya kusafirisha umeme iliyopo kutoka katika chanzo kwenda kwa watumiaji.

“Umeme umesafirishwa kutoka hapa Mtwara kwenda Masasi, Lindi, Mnazi Mmoja hadi Nachingwea kwa kilovoti 32 na kiasi hicho hicho kwenda Tandahimba na Newala, wakati njia hiyo inajengwa mwaka 2006 idadi ya watu ilikuwa ndogo lakini sasa wameongezeka, ni lazima kutakuwa na kukatika katika kwa umeme,” alieleza.

“Isitoshe sababu ya pili  ni kuharibika kwa mtambo wa kuzalisha umeme ambao ulikuwa na uwezo wa kuzalisha megawawti 18, lakini sasa unazalisha megawati 16, huku mahitaji yakiwa ni zaidi ya megawati 17, lakini wakati mtambo huo unajengwa mahitaji yalikuwa ni megawati 12 kwa mikoa ya Lindi na Mtwara,” alisema.

Kuna kila dalili kuwa mahitaji ya umeme yameongezeka mikoa hiyo miwili kutokana na kuongezeka na kukua shughuli mbalimbali  za uchumi kufuatia uwekezaji mkubwa unaowekwa katika mikoa hiyo baada ya kukua kwa shughuli za gesi asilia.

“Tanesco wameshaanza kushugulikia tatizo kwa kuongeza ukubwa wa njia za kusafirishia umeme na kukarabati mitambo na  ili kuitumia gesi kwa matumizi mengine hapo baadaye, tayari mikakati ya kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe na baadaye mabaki ya mimea na njia nyingine imeshaainishwa,” alieleza.

Mkutano ulijadili kwa kina uzoefu uliopatikana katika utekelezaji miradi mikubwa ya gesi kwa mafanikio na kufanya matayarisho kwa miradi mikubwa inayokuja ya Mtambo wa LNG na ule wa kiwanda cha mbolea kitakachojengwa mkoani Lindi eneo la Kilwa.

Wakati huo huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Kapulya Msomba, alisema hadi sasa leseni 11 zimetolewa kwa kampuni zinazojishughulisha na utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles