SERIKALI KUTUMIA MAKAA YA MAWE CHANZO MBADALA NISHATI

0
604

Na MWANDISHI WETU


WIZARA ya Nishati na Madini imewahakikishia Watanzania juu ya upatikanaji wa uhakika wa nishati ya umeme, kwani chanzo chake ni gesi asilia kwa asilimia 50, ingawa lengo la serikali ni kufanya iwe asilimia 40 katika vyanzo vyake.

Imesema kuwa, umeme unapatikana bila tabu kila mahali siku za karibuni nchini kote, kutokana na ukweli kuwa, gesi asilia ndiyo  chanzo chake chenye uhakika na mbadala baadaye ni kutumia makaa mawe kuzalisha umeme nchini.

Kikao cha wadau kilifanyika katika kiwanda cha uchakataji wa gesi Madimba, mkoani Mtwara, ambacho kimehusisha watendaji wa wizara na kampuni zilizowekeza katika utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta nchini, ili kufanya tathmini mbalimbali za sekta hiyo.

Wizara ilisema kuwa, kwa sasa tunazalisha umeme wetu kwa kutumia gesi asilia, ambayo imeimarisha uhakika wa upatikanaji wa umeme ukilinganisha na ilivyokuwa huko nyuma, tulipokuwa tunategemea vyanzo vya maji ambavyo vina matatizo ya kukauka kutokana na  ukame na hivyo kupungua kiasi cha mvua na hivyo maji katika mabwawa mbalimbali.

Iliendelea kusema kuwa, lengo la Wizara ni kupunguza matumizi ya gesi katika kuzalisha umeme hadi ifikie asilimia 40, ili kufanya utegemezi kwenye gesi kupungua na kuleta urari katika vyanzo vya nishati.

Ilisema kuwa, hali hiyo inawezekana tu baada ya kuanza kutumia makaa ya mawe kuzalisha umeme, lakini haukutolewa ufafanuzi lini umeme kutokana na makaa ya mawe utaanza kuzalishwa nchini. Taarifa zilizopo ni kuwa, kuna mradi mkubwa wa nishati kutoka makaa ya mawe kule mkoani Ruvuma, mjini Mbinga, ambapo kampuni ya TANCOAL ina mpango wa kuzalisha umeme wa megawati 250 hadi 300.

“Mipango ya serikali ni kuona kunakuwa na umeme wa uhakika unaotosha kwa matumizi yote ya viwandani na majumbani, ili kusaidia kuharakisha kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi na kulipeleka taifa katika uchumi wa kati wa viwanda kufikia mwaka 2025,” ilisema taarifa.

Tanzania ikishajenga mtambo wa LNG kule Lindi inategemea kuuza nje ya nchi sehemu kubwa ya gesi yake asilia na inategemea kujenga kiwanda kikubwa cha mbolea na hivyo ni muhimu kutafuta aina nyingine ya nishati ili kutumia vizuri rasilimali zake.

Ili kuhakikisha lengo la umeme wa uhakika linatimia, serikali imeweka mikakati kadhaa, ikiwa ni pamoja na kupanua njia za umeme, kuimarisha mitambo ya uzalishaji na kuboresha miundombinu ambayo imechakaa na kutumia rasilimali nyingine katika kuzalisha umeme.

Kwenye swali la kwa nini umeme unakatika mara nyingi mkoani Mtwara na Lindi pamoja na kutumia umeme wa gesi asilia unaodaiwa umeimarika, Wizara ilisema zipo sababu kadhaa za kiufundi zinazosababisha hali hiyo, ikiwamo njia ndogo ya kusafirisha umeme iliyopo kutoka katika chanzo kwenda kwa watumiaji.

“Umeme umesafirishwa kutoka hapa Mtwara kwenda Masasi, Lindi, Mnazi Mmoja hadi Nachingwea kwa kilovoti 32, na kiasi hicho hicho kwenda Tandahimba na Newala, sasa wakati njia hiyo inajengwa mwaka 2006, idadi ya watu wanaohitaji ilikuwa ndogo, lakini sasa wameongezeka, ni lazima kutakuwa na kukatika katika kwa umeme.

“Isitoshe, sababu ya pili  ni kuharibika kwa mtambo wa kuzalisha umeme ambao ulikuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 18, lakini sasa unazalisha megawati 16, huku mahitaji yakiwa ni zaidi ya megawati 17, lakini wakati mtambo huo unajengwa mahitaji yalikuwa ni megawati 12 kwa mikoa ya Lindi na Mtwara.”

Kuna kila dalili kuwa mahitaji ya umeme yameongezeka mikoa hiyo miwili kutokana na kuongezeka na kukua shughuli mbalimbali za uchumi, kufuatia uwekezaji mkubwa unaowekwa katika mikoa hiyo baada ya kukua kwa shughuli za gesi asilia.

“TANESCO wameshaanza kushughulikia tatizo kwa kuongeza ukubwa wa njia za kusafirishia umeme na kukarabati mitambo na ili kuitumia gesi kwa matumizi mengine hapo baadaye, tayari mikakati ya kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe na baadaye mabaki ya mimea na njia nyingine imeshaainishwa,” ilieleza  Wizara.

Mkutano ulijadili kwa kina uzoefu uliopatikana katika utekelezaji miradi mikubwa ya gesi kwa mafanikio na kufanya matayarisho kwa miradi mikubwa inayokuja ya Mtambo wa LNG na ule wa kiwanda cha mbolea kitakachojengwa mkoani Lindi eneo la Kilwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here