Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbas amesema Desemba, mwaka huu wizara hiyo itatoa ripoti ya ongezeko la watalii ambayo imevunja rekodi ya ongezeko la watalii nchini.
Akizungumza leo Julai 8, jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea mabanda mbalimbali kwenye maonyesho ya 47 ya biashara kimataifa sabasaba ya wizara hiyo, Dk Abbas amesema kwa takwimu za nusu mwaka Januari hadi Juni, mwaka huu kumekuwa na watalii wengi kiliko miaka ya nyuma.
“Ongezeko la watalii limetokana na ubunifu wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wa kutengeneza filamu ya The Royar Tour ambayo imesambazwa ulimwenguni kote na kusababisha watu kuiona Tanzania na vivutio vilivyopo ndani yake na wataendelea kutengeneza filamu zingine zinazohusiana na utalii,” amesema Dk. Abbas.
Amesema hadi kufikia mwaka 2025 lengo ni kuwa na watalii milioni 5 na kwamba hadi sasa wamefikia watalii milioni 2.5 ambao ni wa ndani na wa nje milioni 1 hivyo jumla yote kuna watalii milioni 3.5.
Amesema awali kulikuwa na changamoto ya watalii kutofika nchini lakini baada ya kutangaza Royal Tour kuna watalii wengi ambao wanasababisha Taifa kupata fedha za kigeni.
Aidha, amesema wapo kwenye mazungumzo na Tantrade ili mabanda ya wanyamapori yawe endelevu kwa siku zote sio siku ya maonyesho ya sabasaba pekee.
Alisema kutokana na uhaba wa hoteli sehemu za hifadhi na mbugani wapo kwenye mkakati kila eneo hilo kujengwe makazi ili watalii wapate sehemu ya kuishi wanapokuja kufanya utalii na wanawakaribisha wadau kuwekeza.
“Utalii unachangia asilimia 25 ya pato la taifa na hiyo inasaidia kuajiri vijana wengi nchini,” amesema.
Amesema wizara inataka kuboresha mabanda yao kwa sababu yamekuwa kivutio katika maonyesho hayo.
Amesema utalii siyo wanyamapori tu kila kitu ni utalii, sekta ya nyuki, nyumba za kale na misitu ni muhimu.