23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Serikali kutoa kipaumbele sekta binafsi

ARODIA PETER-DODOMA

WIZARA ya Viwanda na Biashara imesema mwelekeo na vipaumbele vya bajeti kwa mwaka wa fedha 2019/20 ni pamoja na kuifanya sekta binafsi kuwa injini ya uchumi.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda, alipokuwa akisoma hotuba ya bajeti yake bungeni ambapo bunge limuidhinishie Sh bilioni 100.38, kiasi ambacho ni pungufu ta Sh bilioni 48.88 ikilinganishwa na bajeti inayoisha.

Kakunda alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuhakikisha wadau wote wanatoa mchango unaohitajika katika ujenzi wa uchumi wa Taifa.

Alisema pamoja na mazingira rafiki ya uwekezaji katika viwanda na biashara, utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara (blue print) unaangaliwa kuwa sehemu ya tiba ya changamoto ambazo zinaitatiza sekta binafsi.

“Hivyo ni mategemeo ya Serikali kuona sekta binafsi inachukua nafasi yake na kuchangamkia fursa zilizopo za kuzalisha na kutoa huduma ikiwa ni hatua muhimu ya kutambua jitihada za Serikali katika kutatua matatizo wanayokabiliana nayo,” alisema.

Kakunda aliitaja miradi ya kimkakati kuelekea ujenzi wa viwanda mama kuwa ni pamoja na Mchuchuma na chuma cha Liganga.

Alisema miradi hiyo inatekelezwa na Kampuni ya Tanzania China International Mineral Resources Limited ambayo ni ya ubia kati ya Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na Schuan Hongda Group ya China.

Kipaumbele kingine alikitaja kuwa ni kufufua kiwanda cha matairi Arusha, maarufu General Tyre kilichokuwa GTEA na utafiti wa kina juu ya ufufuaji huo umeshakamilika.

“Baada ya matangazo kutolewa kupitia tovuti ya NDC, wawekezaji mbalimbali wamejitokeza ikiwamo Kampuni ya Sayinvest Overseas (T) Limited ambayo imeonesha nia ya dhati ya kuwekeza katika uzalishaji matairi nchini.

“Aidha Serikali itaendeleza mradi wa mashamba ya mpira mikoa ya Morogoro na Tanga ambapo NDC imepanda miche takribani 85,250 katika eneo la wazi katika shamba la Kalunga na hadi kufikia Desemba 2018 hekta 155 zilikuwa tayari zimepandwa.

“Mradi mwingine ni uchimbaji wa magadi soda katika Bonde la Engaruka, Wilaya ya Monduli unaohusu kiwanda cha kuzalisha magadi hayo tani milioni moja kwa mwaka kwa matumizi ya viwanda vya dawa, vioo na sabuni,” alisema.

WABUNGE

Mbunge wa Nzega Mjini Hussein Bashe (CCM), alisema kuna ukiritimba katika utoaji wa vibali kwa wawekezaji wanaoanzisha viwanda nchini.

 “Biashara yoyote duniani ina mambo makubwa mawili, na ninachoshukuru Mungu, Rais (John) Magufuli alipoingia madarakani aliweka ‘vision’ yake ‘clear’ ya kutaka kujenga nchi yenye uwezo wa kujitegemea ya viwanda.

“Hii ndiyo ‘vision’, ni matarajio yangu mimi na wengine wote tuliomo humu na Watanzania, kwamba wasaidiaji wanamsaidia mheshimiwa Rais kusaidia utekelezaji wa ‘vision’ hiyo.

“Biashara ina mambo mawili, moja ni ‘software party of business’ na upande mwingine ni ‘hardware part of business’, kwenye ‘hardware party of business’ tunajenga barabara, tunajenga reli, tunanunua ndege na tunajenga miundombinu ya umeme, lakini hii ‘hardware party’ ya biashara isipokuwa ‘compatible’ na ‘software party’ ya biashara ambayo ni ‘regulations’ na sheria, hii itakuwa ni ‘wastage’ ya ‘resources’.

“Kama tutajenga reli, barabara tutaleta umeme vyote hivi vikakosa biashara ya kuvifanya viwe ‘effective’, havitakuwa na maana.

“Nitoe mifano michache, kwenye kamati yetu ya bajeti walikuja watu wa CTI, kwenye ‘presentation’ yao wanasema hivi, ‘unakuta taasisi 15 ‘zina-regulate food processing industry, pharmaceutical industry’ ili aanzishe kiwanda kidogo cha ‘pharmacy’ anahitaji jumla ya leseni 26, ili aweze kuanzisha mradi.

“Kampuni inayotaka kufanya biashara ya maua na bidhaa zingine anahitaji jumla ya vibali 45,” alisema Bashe.

Katika hatua nyingine, Bashe alishauri Serikali kutumia taarifa ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambayo ilitoka awali kwa sababu ina ushauri mzuri.

Alisema taarifa hiyo inatoa ushauri kwamba kama Tanzania inataka kukuza uchumi kwa asilimia 7, kuna mambo manne ya kufanya.

Mbunge wa Monduli, Julius Karanga (CCM) alisema hakuna ushirikiano kwenye wizara za Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

Alisema wananchi wa Monduli walitoa ardhi kwenye mradi wa magadi ulipo Engaruka, lakini hakuna hata kilometa moja ya barabara kutoka Mto wa Mbu kwenda kwenye eneo la mradi.

“Hivi kuna mwekezaji gani anayeweza kwenda kuchukua magadi wakati hakuna hata kilometa moja ya barabara iliyojengwa kuelekea kwenye mradi. Ni bora muwaambie wananchi wetu waendelee kuyatumia maeneo yao ambayo wameyatoa kwa bei rahisi,” alieleza.

Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby (CCM) alisema; “Kuna kukomoana kwenye biashara, watu wanapigwa faini zisizostahili waziri wa viwanda upo, sasa wewe kazi yako ni nini. Kila mtu siku hizi amekuwa ni mkusanya kodi.

“Mimi nataka nijue, maana ya kuwa waziri ni kukuza biashara, si kuua biashara, nikushauri mheshimiwa waziri ingilia popote ambapo mfanyabiashara anaonewa.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles