-DAR ES SALAAM
SERIKALI imeahidi kuwasaidia wazalishaji wadogo wa bidhaa mbalimbali zikiwamo za ngozi kwa kuwajengea uwezo wa kuzalisha kwa wingi na ubora kuelekea katika ujenzi wa uchumi wa Tanzania ya viwanda.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam juzi na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda, kwenye mkutano wa wazalishaji wa bidhaa za ngozi uliokwenda sambamba na maonyesho ya siku moja ya bidhaa hizo nchini.
Alisema Serikali ya awamu ya tano ina nia ya dhati ya kuwawezesha Watanzania kuumiliki uchumi kwa kuweka mazingira wezeshi na vivutio mbalimbali.
“Serikali ina vipaumbele vya kuwawezesha wazawa kuanzisha viwanda kukuza bidhaa za Tanzania zikiwamo za sekta za ngozi, hivyo mnapaswa kuwa na ujasiri wa kuzalisha na kutumia fursa hiyo kwa ajili ya ushindani,” alisema.
Katibu Mkuu huyo alitumia nafasi hiyo kuwahamasisha wazalishaji hao kutumia soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na soko la SADC kwani wana haki ya kuuza kwenye kanda hizo.
Vile vile aliwaasa kutumia taasisi nyingine za Serikali zinazoweza kuwainua kwenye sekta hiyo kuondokana na changamoto mbalimbali.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Edwin Rutageruka, alisema taasisi yake ipo tayari kuwapa mafunzo ya ujasiriamali wazalishaji hao.