SERIKALI imetangaza mpango wake wa kuwaruhusu wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito kuendelea na masomo ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na ukatili wa kijinsia.
Akizungumza jana katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa jinsia yaliyofanyika jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Paulina Mkonongo, alisema ujauzito ni miongoni mwa sababu za wanafunzi wengi kuacha shule.
“Serikali yetu ina takwimu zinazoonyesha watoto watoro waliopata mimba, wanaonyimwa haki ya kupata mahitaji na sare za shule, vifo na yatima wanaojilea wenyewe. Serikali tunaandaa utaratibu wa wanafunzi waliopata mimba waendelee na masomo,” alisema Mkonongo.
Alisema dira ya elimu ni kuwa na Mtanzania aliyeelimika, mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mtazamo chanya ili kuchangia kuleta maendeleo.
Akitaja juhudi zilizofanywa na Serikali kupambana na ukatili huo, Mkonongo alisema imetekeleza mpango wa taifa wa kutokomeza ukatili na mila zinazoleta madhara katika jamii.
“Ili kutekeleza azma hii, Serikali imeunda kamati ya kitaifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, watoto na albino, inayoratibiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsi na Watoto,” alisema.
Aliitaja pia sera ya taifa ya maendeleo ya mtoto ya mwaka 2008 toleo la pili na sheria ya mtoto ya mwaka 2009 yenye madhumuni ya kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa aina yoyote ile.
Alisema Jeshi la Polisi limeanzisha madawati ya jinsia na watoto kwa ajili ya kuhudumia waathirika wa kijinsia na watoto.
Awali akizungumza katika mkutano huo, Mratibu wa Kitaifa wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo (WiLDAF), Dk. Judith Odunga, alisema ili kuwe na ubora katika elimu, ni lazima usalama wa mwanafunzi uhakikishwe.
“Tunaiomba Serikali kufuta kabisa adhabu ya viboko shuleni na walimu kufundishwa au kutafuta mbinu za kutoa adhabu mbadala,” alisema Dk. Odunga.
Aliitaka Serikali kutengeneza mwongozo wa utekelezaji wa sera ya elimu ya mwaka 2014, utakaoelekeza upatikanaji wa elimu ya msingi iliyo bora na salama.
Aliongeza kuwa Serikali inatakiwa kuboresha miundombinu ikiwa pamoja na madarasa, madawati, vyoo na sehemu za kujisitiri kwa watoto wa kike, mabweni, uzio na usafiri wa uhakika.
Alishauri pia kuwapo kwa mabaraza yatakayosimamia malalamiko ya wanafunzi na wizara za Elimu na Sheria kubadilisha sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu mtoto wa kike chini ya umri wa miaka 18 kuolewa, kwa ridhaa ya wazazi, mlezi au mahakama.
Maadhimisho hayo pia yalihudhuriwa na mtendaji mkuu wa miradi ya maendeleo wa ubalozi wa Ireland, Maire, Matthews, wawakilishi wa asasi za kiraia, walimu na wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari.