23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

SERIKALI KUPIGA MARUFUKU MALORI YA KONTENA DAR

Na Mwandishi Wetu


WIZARA ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, imelivalia njuga suala la kupunguza msongamano sugu wa magari Dar es Salaam, kwa kupunguza yale yanayoingia na kutoka humo haswa  malori ya mizigo ya makontena.

Suala hilo linatekelezwa kwa kujenga bandari kavu nje ya Dar es Salaam katika Mkoa wa Pwani, eneo la Ruvu ili liwe kimbilio la kufanyia kazi za usafirishaji mizigo.

Mradi wa Ujenzi wa bandari Kavu (ICD) ya Ruvu, unatarajia kugharimu kiasi cha Sh bilioni 7.3 katika eneo la ukubwa wa hekta 500 lililoko Ruvu.

Bandari kavu hiyo itakayojengwa Mkoa wa  Pwani, ina lengo la kupunguza msongamano wa malori jijini Dar es Salaam kwa kuyazuia kufanya kazi humo au kulazimisha kufanya kwa kibali maalumu.

Ujenzi huo utakamilika katika kipindi cha wiki tisa na itajengwa na Shirika la Uchumi la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA-JKT).

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, wiki iliyopita alisema mkataba wa ujenzi huo ulishasainiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na SUMA JKT.

Mradi huo utakapokamilika, makontena yote yatasafirishwa kwenda bandari kavu ya Ruvu kwa reli na malori yanayotoka mikoani na nchi jirani, yatakuwa yanachukulia mizigo yao huko.

 “Tunatarajia kuwa ujenzi ukikamilika ndani ya wiki hizo tisa, bandari  kavu hiyo itaanza kufanya kazi,” alisema Mbarawa.

Aliongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi huo, kutaleta ufanisi mkubwa katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa kuwa hakutakuwa tena na msongamano wa makontena.

Mpango wa Serikali ni kuwa bandari kavu zote za jijini Dar es Salaam, zijengwe nje ya mji ili kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji.

Kwa sasa malori  yote haswa ya makontena, hufika bandarini kwa ajili ya kuchukua shehena mbalimbali ambayo huleta usumbufu na msongamano mkubwa wa magari.

Hii inamaanisha magari yote makubwa ya mzigo yataishia Bandari Kavu ya Ruvu.

Aidha, Serikali imeamua kuwapa SUMA JKT kujenga bandari hiyo, kwa sababu ya kuharakisha ujenzi huo kumalizika kwa muda uliyopangwa kwa ufanisi mkubwa.

Alipoulizwa kuhusu umahiri na ubora wa kazi za mkandarasi huyo, waziri alitetea uamuzi huo.

“Sisi hawa hatuwaangalii kama JKT, bali tunawaangalia kama wakandarasi, hivyo tutaendelea kumsimamia kuhakikisha anakamilisha kazi kwa muda tuliokubaliana,” alieleza.

Naye Mwanasheria wa SUMA JKT, Kanali John Mbungo ambaye alisaini mkataba huo kwa niaba ya JKT, alisema TPA waendelee kuwaamini kwani wataifanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles