Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Serikali imeitaka Bodi ya Wakurugenzi ya Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC) kuhakikisha inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kutoa ufadhili wa masomo kwa wataalamu wa masuala ya atomiki ili kuongeza ujuzi katika sekta hiyo muhimu.
Wito huo umetolewa leo Februari 19, 2025, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya TAEC. Waziri Mkenda alisema serikali imetenga fedha kwa ajili ya mafunzo ya muda mrefu katika vyuo vikuu nje ya nchi ili kuendeleza wataalamu wa atomiki na nyuklia.

“Kipaumbele cha kwanza ni kwa watumishi wa TAEC, na cha pili ni kwa wanafunzi wa vyuo vikuu watakaokidhi vigezo. Tukiwapeleka wakasome, tutapata wataalamu wa hali ya juu katika sekta hii,” amesema Profesa Mkenda.
Alifafanua kuwa mpango wa Samia Scholarship Extended utawezesha Watanzania kusoma katika vyuo bora duniani katika masuala ya atomiki na nyuklia ili kuendeleza taaluma hiyo nchini.
Profesa Mkenda pia aliisisitizia Bodi ya TAEC kuhakikisha inasimamia kikamilifu fedha zilizotengwa kwa ajili ya ufadhili huo.
“Twendeni tukajifunze katika vyuo bora mlivyovitambua, nawataka bodi ihakikishe mpango huu unatekelezwa kikamilifu. Mnapewa mamlaka ya kuchagua wanafunzi na kuwapeleka kusoma kulingana na miongozo tuliyotoa,” ameeleza Waziri Mkenda.
Aidha, aliipongeza Bodi ya TAEC kwa kutenga bajeti maalum kwa ajili ya kuwafundisha Watanzania katika vyuo bora vya kimataifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TAEC, Profesa Joseph Msambichaka, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuongoza Bodi hiyo kwa kipindi cha pili tangu Juni 2024.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Najat Mohammed, alisema tume hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kudhibiti na kuhamasisha matumizi ya teknolojia mpya kwa mujibu wa sheria za nchi. Mpango huu unalenga kuimarisha ujuzi wa wataalamu wa atomiki nchini, hatua ambayo inatarajiwa kusaidia maendeleo ya sekta ya sayansi na teknolojia kwa ujumla.