Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Waziri Mkuu Kasim Majaliwa, amesema Serikali itaendelea kuondoa vikwazo vinavyowakabili wanawake kwenye biashara na kuhakikisha kuna ushiriki sawa katika kutumia fursa zitokanazo na eneo huru la biashara barani Afrika.
Ameyasema hayo leo Desemba 6, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la wanawake katika biashara chini ya mkataba wa eneo huru la biashara Afrika litakalofanyika kwa muda wa siku tatu na kuhudhuliwa na viongozi mbalimbali kutoka nchi 55 za Afrika.
Amesema Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambae ndie kinara wa kuhamasisha wanawake katika biashara ndani ya eneo huru la biashara Afrika, imechukua jukumu la kuchangia kikamilifu katika kuharakisha.

“Nchi imeanzisha program ya mpango wa kisekta lengo likiwa kuongeza wadau wa umma,binafsi na kijamii katika miradi inayojumuisha eneo la kiusawa wa kiuchumi ambapo katika progamu hiyo Tanzania imebainisha mapungufu yaliyopo katika usawa wa kijinsia na hatua za kuchukua na kuweka matarajio ya matokeo ya hatua zinazochukuliwa, ” amesema Majaliwa.
Amesema ushiriki wa umakini katika kongamano ni muhimu kwa kila mmoja wao ili kupata mafanikio ya agenda ya kinara Rais Dk. Samia .
Ameongeza kuwa michango ya mawazo ya kongamano hilo yataunda mpango mkakati wa afua zitakazokuwa zinaongoza agenda na kupima matokeo ya utekelezaji kwa niaba ya wanawake wote barani Afrika.
Pia Majaliwa amewataka wanawake wafanyabiashara na wadau mbalimbali kujitokeza kufanyabiasha na kuwekeza nchini lakini pia kutembelea vivutio vilivyopo ikiwemo mbuga za wanyama, fukwe na Mlima Kilimanjaro.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Ashatu Kijaji, amesema wataendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kuwasaidia wanawake kulifikia soko huru la Afrika.
Amesema kongamano litasaidia kutatua changamoto za wanawake katika biashara, kuimarisha na kukuza mchango wao kwenye biashara na uchumi.
“Tayari tumekamilisha mkakati wa kitaifa wa utekelezaji wa eneo huru la biashara Afrika ambao tunategemea kuuzindua mapema mwanzoni mwa mwaka 2024 pamoja na kamati ya kitaifa ya kusimamia utekelezaji wa mkakati huo,”amesema Dk.Kijaji.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu , Dk.Dorothy Gwajima amesema majukwaa ya wanawake katika biashara yanatoa fursa ya kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto yanayowanyima fursa ya kujiendeleza kiuchum
Amesema serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa asasi za kiraia na wadau wote wa maendeleo katika kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Kongamano la wanawake katika biashara chini ya mkataba wa eneo huru la biashara Afrika ni kongamano la pili kufanyika nchini ambapo kongamano la kwanza lilifanyika Septemba 12-14, 2022 jijini Dar es Salaam na kuhudhuliwa na watu 1060 kutoka nchi mbalimbali Afrika.
Kongamano hilo lililenga kuwakutanisha viongozi wakuu wanawake,mawaziri wanawake wajasiliamali na wadau mbalimbali lengo likiwa kujadili,kutoa maoni,ushauri na mapendekezo ya kuwezesha uandaaji itifaki kwa ajili ya kuwezesha wanawake na vijana kushikiriki kikamilifu katika biashara ndani ya Afrika.
Pamoja na kufanikiwa kwa itifaki hiyo kongamano hilo lilitoa njia sahihi ya kutatua vikwazo na changamoto zinazowakabili wanawake na vijana katika biashara ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika biashara barani Afrika ikiwa ni pamoja na upatikanaji mdogo wa fedha,taarifa za masoko,pembejeo,matumizi ya teknolojia,masoko,uwezo mdogo wa kufuata viwango na mahitaji mengine ya kisheria.