NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kutangaza ununuzi wa rada sita za kisasa kwa ajili ya kuboresha usimamizi na ufuatiliaji wa safari za anga.
Kauli hiyo aliitoa mjini Unguja jana baada ya kukagua shughuli zinazofanywa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) na Uwanja wa Ndege wa Zanzibar na alisisitiza umuhimu wa kufuata sheria katika kumpata mzabuni.
“Tumejipanga kuhakikisha miundombinu ya safari za anga nchini inaimarika ili kuvutia utalii na usalama wa abiria wa usafiri wa anga,” alisema Profesa Mbarawa.
Aliitaka TCAA kuhakikisha marubani wanaopewa vibali vya kurusha ndege nchini wanakidhi vigezo vya kimataifa ili kuufanya usafiri wa anga kuwa salama.
Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Balozi Ali Abeid Karume, alimpongeza Profesa Mbarawa kwa ushirikiano anaoufanya kati ya wizara hizo kwa kuwa inaongeza ufanisi.
“Huduma wanazozipata Bara ni vyema na sisi Zanzibar tukanufaika nazo ikiwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano ili kuleta usawa kwa wananchi wa pande zote za Muungano,” alisisitiza Balozi Karume.