26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali: Kuna upungufu wa asilimia 60 ya watumishi wa afya

*Kuongezeka kwa vituo vya afya kwatajwa kama sababu

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Serikali imebainisha kuwa bado kuna upungufu wa takribani asilimia 60 ya watumishi wa afya nchini pengo linalochangiwa na kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma za afya.

Hayo yamebainishwa leo Dar es Salaam Jumanne Septemba 12, 2023 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Grace Maghembe, kando ya mkutano uliokutanisha wadau mbalimbali ukiangazia namna ya kukabiliana na upungufu wa watumishi katika sekta ya afya nchini.

Amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kumekuwa na mwamko mkubwa wa kuboresha huduma za afya nchini ikiwamo ujenzi wa vituo na vifaa tiba.

“Sasahivi upungufu wa watumishi wa afya ni mkubwa kidogo karibia asilimia 60 na hii imetokana na maendeleo ambayo tumeyafanya kwani katika kipindi hiki cha miaka miwili na nusu kumekuwa na uwekezaji mkubwa sana katika sekta ya afya hususan ujenzi wa vituo, kwa hiyo kadri unavyoongeza vituo vya kutolea huduma na mahitaji ya watumishi yanaongezeka.

“Kwa hiyo ni kitu kizuri tunafurahia, hospitali zinajengwa, zahanati na vituo vya afya kila sehemu, vilevile tunaona kwamba Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan tangu ameingia madarakani amewekeza sana kwenye vifaa tiba, tumenunua MRI zakutosha ambapo kwa sasa nchini zimefika tano kutoka mmoja iliyokuwepo miaka ya nyuma.

“Ukiacha hilo, sasahivi kuna mashine za CT Scan karibu kila hospitali za mikoa, tuna mashine za X Ray zaidi ya 200, sasa maeneo haya kadri unavyoboresha na mahitaji ya watumishi yanaongezeka na siyo tu watumishi bali amesoma kitu gani hivyo baada ya kuliona hilo ndiyo maana tukaona kwamba lazima tukae pamoja kama Serikali na wadau wote ambao wanahusika na masuala ya watumishi wa sekta ya afya,” amesema Dk. Maghembe.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Grace Maghembe.

Akizungumzia kikao hicho ambacho kimeratibiwa na Taasisi ya Benjamini Mkapa kwa kufadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) amesema kuna Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais Tamisemi, Wizara ya Fedha wawakilishi wa utumishi na wadau wa maendeleo.

“Hiki ni kikao ambacho kimeleta wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa tunakabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi wa afya katika sekta ya afya nchini.

“Tunajua idadi ya watumishi tulionao lakini pia tunaangalia mahitaji halisi ambayo yametusukuma kujua ambacho hatuna na tumekwenda mbele na kusema kwamba hoja isiwe tu idadi bali ni nani hasa tunayemtaka.

“Pili ni kujua kwenye hawa waliopo je wamepangwa vizuri kama wanavyohitajika kabla ya kuomba hao wengine tunaohitaji, hata hivyo ndani ya miaka miwili Mhe Rais Samia  katika kipindi bhiki cha miaka miwili ameajiri watumishi wa afya 10,000 na asilimia 80 ya hao wote wanapelekwa kwenye vituo ambavyo ni vya ngazi ya msingi kwani kule ndiko kulikona wananchi wengi,” amesema Dk. Maghembe.

Katika hatua nyingine amesema Wizara ya Afya inamkakati wa kuajiri watumishi ngazi ya jamii 150,000 katika kipindi cha miaka mitatu ambao watasaidia kutoa elimu kuhusu magonjwa mbalimbali yanayozuilika.

“Tumekuwa na utaratibu wa watu kujitolea hatua ambayo inajenga uzalendo kwa nchi na fursa ya kuongeza ujuzi kwani tunapokuwa na nafasi za ajira huwa tunawapa kipaumbele watumishi hao na mfano mzuri ni wale wanaojitolea kupitia taasisi ya Benjamini Mkapa ambapo wengi wameajiriwa na serikali,” amesema Dk. Maghembe.

Amesema hakuna mafanikio ambayo yanakuja kwa kutegemea Serikali peke yake na kwamba wadau hususan sekta binafsi wanapaswa kushirikiana na Serikali katika kufikia malengo ya kuwa na huduma bora za afya.

Akizungumzia kikao hicho na ushiriki wao Mkurugenzi anayesimamia masuala ya Mikakati, Utendaji na Mifumo Taasisi ya Benjamini Mkapa, Dk. Mussa Ndile, amesema wanafurahi kushirikiana na Serikali katika kunyanyua sekta ya afya nchini.

“Lengo ni kuona kuwa tunaweka mchango wetu kwenye raslimali watu katika sekta ya afya hususan katika maeneo yasiyofikika na yenye huduma ambazo hazifikiki kwa wakati na wahitaji, hivyo kikao hiki ambacho kinaratibiwa na taasisi yetu kinalenga kuwashirikisha wadau wenzetu wa maeneo haya ya raslimali watu katika sekta hii ya afya kuhakikisha kwamba tunapitia mkakati ambao tumekuwa tukijiwekea siku za hivi karibuni wa kuhakikisha kwamba Watanzania ambao wanahitaji huduma za afya wanafikiwa na hasa katika maeneo ambayo tunaunga mkono juhudi za Serikali hususan zahanati mpya na vituo vya kutolea huduma za afya.

“Pia huduma za kibingwa bobezi, hivyo tunawashukuru wadau ambao wamekuwa na sisi leo na wananchi, tunafarijika tunapoona kwamba huduma zinawafikia watumishi wenzetu na tuendelee kuungwa mkono watumishi tunaowapeleka kwenye vituo wapewe mazingira mazuri ya kazi na nafasi zinapotokea za kuendeleza ujuzi wao basi wapewe.

“Rai yetu kwa Serikali ni kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wadau mbalimbali katika kuchangia juhudi za serikali katika kuharakisha upatikanaji wa raslimali watu na huduma za afya,” amesema Dk. Ndile.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles