Na TUNU NASSOR -DAR ES SALAAM
OFISI ya Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, imesema inafanya mawasiliano na Mama mdogo wa Mwanafunzi Anna Zambi, aliyefiwa na wazazi wake pamoja na wadogo wake watatu, kujua shule anayotaka ili waweze kutimiza ahadi yao ya kumtafutia shule ya bweni.
Anna alipoteza wazazi wazazi pamoja na wadogo zake ambao walikuwa anakwenda kuhudhuria sherehe za mahafali yake ya kuhitimu Kidato cha Nne, ambapo alifanya mitihani pasi na kujua kama ni yatima.
Kwa mujibu wa matokeo ya yaliyotangazwa Januari 8, mwaka huu na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Anna aliyehitimu Shule ya Sekondari ya Mother Theresia of Calcuta mkoani Kilimanjaro, amefaulu kwa kupata daraja la pili pointi 20.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Hamisi Lissu, alisema kwa sasa ofisi yake wanafanya mawasiliano na mama yake mdogo Anna ili kufanya uchaguzi wa shule anayotaka kwenda.
Alisema ofisi yake itasimamia maendeleo ya binti huyo kwa kuwa waliahidi kumtafutia shule anayotaka na kusimamia mahitaji yake.
“Kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, tutahakikisha anapata shule nzuri ya bweni na kusimamia mahitaji ili aweze kusoma bila kukwama,” alisema Lissu.
Aidha alisema mkoa huo unafanya tathmini kujua sababu ya shule zake za sekondari kushindwa kufanya vizuri katika mtihani huo wa kidato cha nne.
Alisema kwa miaka miwili mfululizo Mkoa wa Dar es Salaam, umekuwa haumo katika orodha ya shule 10 bora.
“Mwaka 2018 tulishika nafasi ya 16 kati ya mikoa 31, katika matokeo ya mwaka jana yaliyotangazwa hivi karibuni tumeshika nafasi ya 18, tutakutana kujitathimini kwa nini hatuingii katika kumi bora kama yalivyo matokeo ya darasa la nne, saba na Kidato cha pili,” alisema Lissu.
Alisema katika tathmini hiyo watapitia maswali ambayo wanafunzi hawakufanya vizuri ili kujua sababu za msingi zilizosababisha.
“Kwa kufanya hivyo tutaweza kubaini iwapo walimu tulionao wana uwezo wa kutosha katika kufundisha masomo hayo,” alisema Lissu.
Alisema mkoa huo umeshika nafasi ya kwanza kitaifa kwa mtihani wa darasa la nne, mtihani wa kidato cha pili uliingia katika kumi bora na kidato cha nne ukishika nafasi ya 18.