Na MWANDISHI WETU-UYUI
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Serikali italipa madeni yote ya watumishi wa umma ambayo yamehakikiwa na kuonekana ni halali.
Waziri Mkuu Majaliwa, aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Mkoa wa Tabora, kwenye mkutano uliofanyika Kata ya Goweko, wilayani Uyui, mkoani hapa.
“Mheshimiwa Rais, Dk. John Magufuli, alisitisha malipo kwa sababu ya zoezi la kubaini watumishi hewa. Sasa kazi hiyo imekamilika, yale yaliyobainika kuwa ni halali yatalipwa kwa sababu tunataka watumishi mfanye kazi ya kuwahudumia wananchi kwa bidii,” alisema Waziri Mkuu.
Akiwa katika wilaya za Sikonge, Urambo, Kaliua na Uyui, Waziri Mkuu alielezwa na baadhi ya wabunge wa mkoa huo kwamba kuna watumishi ambao walihamishwa kutoka manispaa kwenda wilaya za jirani lakini hawajalipwa fedha zao kwa zaidi ya miaka mitano sasa.
Kwa nyakati tofauti, Waziri Mkuu ambaye ameweka utaratibu wa kukutana na watumishi wa umma kila anapofanya ziara za kikazi mikoani, aliwaeleza watumishi wa wilaya hizo kwamba Serikali imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma ambao unalenga kuondoa tatizo la madai ya malimbikizo ya stahili zao.
“Hivi sasa tunadhibiti uzalishaji wa madeni mapya ya watumishi, hakuna madeni ya matibabu, madeni ya likizo au ya masomo.
“Kila mtumishi anaruhusiwa kujiendeleza, lakini ni lazima kwanza aandike barua kwa mkurugenzi wa halmashauri kuelezea nia yake na akikubaliwa, ndipo aanze kutuma maombi kwenye vyuo.
“Mtumishi akiamua kuomba chuoni moja kwa moja ndipo alete madai yale, hatapewa chochote kwa sababu ni nje ya utaratibu,” alisema.
Akifafanua utendaji kazi wa mfumo huo, Waziri Mkuu alisema mfumo huo ujulikanao kama LAWSON, unatumika kwenye ajira za watumishi wote nchini, Serikali Kuu na wale wa Serikali za Mitaa na kwamba unasaidia kutunza, kutuma na kuhuisha taarifa za watumishi kwa wakati na kwa ufanisi tangu mtu anapoajiriwa hadi inapofikia wakati wa kupandishwa madaraja ama kustaafu.