WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imetangaza mkakati wa ukaguzi wa dawa zinapoingia katika Bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni mkakati wa kuzuia upotevu.
Imesema imeandaa mpango unaojulikana kama ‘Pilferage Tool’ ambao utatumika kufanya ukaguzi wa upotevu wa dawa unaosadikia kutokea kuanzia mzigo unapoingia bandarini mpaka kumfikia mgonjwa.
Mkakati huo ulitangazwa jana bungeni mjini hapa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alipowasilisha bajeti ya wizara yake ya Sh bilioni 277.6.
Alisema mfumo huo utasaidia upatikaji wa dawa kwa hospitali zote nchini.
Waziri alisema pia kuwa Serikali imefanya mapitio ya kina ya mfumo wa ununuzi na utunzaji wa dawa katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
“Ili kuepuka kulipa kodi na tozo zilizo juu kutokana na misaada inayoletwa nchini bila kuwa na utaratibu maalumu wa kupokea misaada hiyo.
“Wizara itatoa mafunzo ya kusambaza na kusimamia utekelezaji wa mwongozo wa ufanisi wa kazi kupitia mfumo wa 5S Kaizen TQM kuimarisha usimamizi wa takwimu za dawa,” alisema Ummy.
Alisema wizara imeendelea kuboresha huduma ya afya ya uzazi na motto na katika mwaka 2015/16 iliwajengea uwezo watoa huduma jinsi ya kumhudumia mtoto aliyezaliwa na upungufu wa uzito.
Licha ya hali hiyo suala la vifo vinavyotokana na uzazi bado ni changamoto ambako kutokana na taarifa za Umoja wa Mataifa (UN), Tanzania imepunguza vifo hivyo kutoka 454 mwaka 2010 hadi 398 mwaka 2015.
“Ili kuhakikisha vifo hivi vinaendelea kupungua kwa kasi zaidi wizara imehakikisha watoa huduma wa afya 2,087 wamejengewa uwezo kwa kuwapatia mafunzo ya huduma muhimu wakati wa ujauzito, stadi za kuokoa maisha kwa matatizo ya dharura yatokanayo na mtoto mchanga na baada ya kujifungua,” alisema.
Akizungumzia huduma za chanjo, alisema wizara itaendelea kutoa miongozo ya huduma za chanjo kulingana na miongozo.
“Pia Wizara imeendelea na juhudi za kudhibiti UKIMWI kwa kutoa ushauri nasaha na kupima na kuanzia Januari hadi Desemba mwaka jana, wateja wapya 3,474,780 walipata ushauri nasaha na kupima VVU.
“Na idadi hii inajumulisha pia waliopata huduma kupitia mpango wa kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto PMTCT,” alisema.
Maoni ya upinzani
Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Msemaji wa Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Godwin Mollel, alisema suala la upungufu wa madawa unaweza kuongezeka kwani Serikali imetenga Sh bilioni 65.1 kwa ajili ya ununuzi wa dawa.
Alisema kiasi hicho kinatosha mahitaji ya nchi kwa mwezi mmoja na nusu tu kwa kukadiria kuwa Tanzania ina watu takribani milioni 49.8 wanaohitaji matibabu, kiasi kilichotengwa kinatosha kutibu watu milioni 5.6 kwa mwaka.
“Je, watu wengine milioni 44 wanaobaki watatibiwa na nini na wapi? Mheshimiwa Spika: Kambi Rasmi ya Upinzani inaishauri Serikali iongeze bajeti ya madawa kutoka asilimia 11 (bilioni 65.1) mpaka angalau asilimia 50 ya mahitaji (bilioni 295.9).