Na MWANDISHI WETU
-KIBAHA
SERIKALI imeanza ujenzi wa hospitali mpya ya kisasa katika eneo la Kata ya Picha ya Ndege kwa lengo la kuwaondolea kero wananchi ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
Akizungumza jana na kuhusiana na ujenzi huo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Lulanzi inapojengwa hospitali hiyo, Thobiasi Shilole , alisema kukamilika mradi huo kutaweza kuwa ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya Kibaha.
Alisema hiyo ni kwa kuzingatia kuwa awali walikuwa wanapata usumbufu mkubwa wanapohitaji huduma ya matibabu.
Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka (CCM), ambaye alifanya ziara ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo, alimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kuamua kutoa Sh bilioni 1.5 ya ujenzi huo.
Aliwataka wakandarasi kuhakikisha wanajenga majengo yenye ubora unaotakiwa na kuachana na tabia ya kufanya kazi ambazo zipo chini ya kiwango.
Koka alisema kutekelezwa kwa mradi huo ni kutokana na juhudi ambazo alizifanya kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wa wilaya pamoja na serikali kuu kwa ujumla.
Aliahidi kuendelea kuleta maendeleo kwa wananchi katika sekta mbalimbali.
“Huu mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya kwa kweli umeletwa kwetu kwa lengo la kuwasaidia wananchi katika suala zima la kuwasogezea huduma ya matibabu.
“Kwa hivyo ninatoa pongezi zangu za dhati kwa Rais wa awamu ya tano, Dk. John Magufuli katika kuwaboreshea wananchi huduma ya afya pamoja na mambo mengine,” alisema Koka.
Diwani wa Kata ya Picha ya Ndege, Robert Machumbe (CCM), alisema serikali ya Awamu ya Tano inawaletea wananchi mabadiliko chanya ya maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Alisema kwa sasa limepatikana eneo la ekari 25 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya.
“Kwa kweli tunapenda kuishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuweza kutuletea mabadiliko chanya ya maendeleo.
“Utaona kwa sasa katika kata hii ya picha ya ndege kuna hatua kubwa ambayo tumeifanya katika nyanja mbalimbali na sasa tumeshaanza ujenzi wa hospitali yetu ya wilaya.
“Hospitali itajengwa katika mtaa wa Lulanzi kwa hivyo hii ni hatua kubwa pamoja na shule ya sekondari ambayo tayari eneo la ekari 11.7 limekwisha kupatikana,” alisema.